Tangu ugonjwa wa homa ya dengue uibuke mkoani Dar es Salaam na baadaye maeneo mengine ya nchi, wananchi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi yenye utata ambayo sasa yamepata majibu ya wataalamu.
1. Kwa nini mbu wengine wakiwamo wanaoambukiza malaria hawawezi kuambukiza dengue?
Mtafiti wa tabia za mbu kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Nicholaus Govela alisema mbu anayeambukiza homa ya dengue, Aedes Egypti, hawezi kubeba vimelea vya malaria wala yule anayeambukiza malaria hawezi kuambukiza dengue kutokana na maumbile yao.
Dk Govela alisema fiziolojia ya mwili wa mbu haiwezi kuruhusu Aedes Egypti kubeba virusi vya mbu mwingine.
“Ndiyo maana mbu hawezi kuambukiza Virusi vya Ukimwi,” alisema.
2. Kwa nini mbu wa dengue huuma mchana?
Dk Govela alisema suala hilo bado linahitaji utafiti zaidi kwa sababu kati ya aina tatu za mbu wanaosababisha dengue, hakuna utafiti uliofanyika kujua tabia zao wote.
Aina hizo ni Aedes Egypti, Aedes Albokictus na Aedes Africaans.
Alibainisha kuwa katika tafiti zinazofanyika, IHI iliwahi kubainika kuwa Aedes African ambaye pia anaambukiza dengue huuma usiku.
Alisema wengi wanamwelezea mbu huyu kwa kumlinganisha na tabia za mbu wa Japan, China na America ya Kusini lakini inawezekana huyu aliyepo hapa ni mpya tofauti na wa nchi za nje.
3. Je, dawa inayopulizwa inafaa kuwaangamiza?
Dk Govela alisema inawezekana ndiyo au hapana, lazima hili pia lifanyiwe utafiti kwa kuwa upo uwezekano wa mbu hawa kujenga usugu wa dawa kwa kuwa wamekuwapo nchini kwa miaka mingi.
Alipongeza uamuzi wa Serikali wa kupuliza dawa kwenye mabasi ya mikoani lakini bado alihoji iwapo imefikiria udhibiti kuanzia katika viwanja vya ndege na iwapo itawezekana kuzuia watu wanaokwenda mikoani wakiwa tayari wameambukizwa.
4. Je, kuna watu wanaougua dengue bila kuonyesha dalili?
Mtafiti huyo alisema wapo wanaougua bila kuonyesha dalili na wanaendelea kuambukiza... “Hawa mara nyingi hawaendi hospitali lakini wanakuwa na virusi mwilini,” alisema.
5. Kuna aina ngapi za virusi vya dengue?
Dk Govela alisema zipo aina nne za virusi vinavyoambukiza dengue. Alivitaja kuwa ni den 1, den2, den 3 na den 4. Hadi sasa, wanasayansi hawajaweza kubaini ni virusi vya aina gani vinasababisha homa hiyo kwa Tanzania.
“Ndiyo maana tunahitaji kufanya tafiti zaidi,” alisema.
6. Je, juisi ya majani ya papai ni tiba ya dengue?
Ofisa wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Grace Saguti alisema haijathibitishwa kisayansi.
Dk Saguti alisema ili tiba ikubalike, lazima ithibitishwe na hakuna namna mbadala ya kuiruhusu itumike kabla ya kujua madhara na faida zake. Alisema mpapai unaongeza vitamini A na hivyo kuimarisha kinga ya mwili, lakini si kutibu virusi vya dengue ambavyo kwa asili yake havina dawa.
7.Mbu wa dengue wako Dar es Salaam pekee?
Mtaalamu wa IHI alisema mbu huyo anaishi katika maeneo ya kitropiki, hivyo huenda yupo hata katika mikoa mingine. Alisema kwa tabia, aedes africans anafanana na mbu aina ya culex ambaye anapatikana katika mikoa mingine, hivyo hata huyo anaweza kuwapo huko pia... “Lazima ufanyike utafiti ili tujue iwapo mbu huyo hawezi kuzaliana katika mikoa mingine,” alisema.
8. Kwa nini aedes hupenda maji masafi yaliyotuama?
Dk Govela alisema ni kutokana na asili ya maumbile yao. Mbu hao huamini maji masafi yaliyotuama huwapa joto zaidi kwa ajili ya kutaga mayai.
“Lakini si lazima wawe wanazaliana zaidi katika maji masafi kwa sababu wana tabia ya kubadili tabia. Kwa mfano, anopheles wanaoeneza malaria nao walipenda maji masafi awali, lakini kwa sasa wamebadilika wanazaliana hata kwenye maji machafu,” alisema
9.Kwa nini wahudumu wa afya wanaathirika zaidi?
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa Homa ya dengue, Mrisho Lupinda alisema nao ni binadamu kama wengine na wanaishi maeneo hatarishi yenye mbu kama watu wengine.
10. Kwa nini panadol pekee ndiyo inatibu dalili za dengue?
Dk Lupinda alisema dawa nyingine za maumivu yaani Diclopar, Diclofenac na Aspirini huingiliana na mfumo wa chembe hai nyeupe za damu na huweza kusababisha chembe hizo kupungua mwilini. Dawa hizo huchochea kutengeneza sumu ambayo huathiri baadhi ya ogani za mwili.
Ugonjwa wasambaa
Homa ya dengue imesambaa katika maeneo mbalimbali nchini na kutoka Shinyanga, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Fredrick Mlekwa amesema kumetokea kifo cha mtoto aliyekuwa na dalili zote za ugonjwa huo.
Huko Arusha, mkazi wa Maji ya Chai, Frank Nnko (30) amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru akitokea Hospitali ya Wilaya ya Meru akiwa na dalili za homa hiyo.
Zanzibar, wagonjwa watatu wanaodhaniwa kuwa na homa ya dengue wamelazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja. Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema wagonjwa hao wana dalili za ugonjwa huo.
Mtu mmoja amelazwa katika Hospitali ya Tumbi akiwa na dalili za dengue, akiwa na maumivu ya kichwa na kutoka damu puani, Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Gerald Chami alisema mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 30, alitokea Mbezi Wilaya ya Kinondoni.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment