Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Stephen Wassira
amewatisha wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwamba
wasiporejea bungeni, kanuni zitabadilishwa na Bunge litaendelea.
Wassira alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu hoja za wabunge
mbalimbali akiwamo Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuwa
majadiliano ndani ya Bunge la Katiba yanakiuka Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba.
Katika mchango wake, Mdee alisema Ukawa hawako tayari kurejea ndani
ya Bunge Maalumu la Katiba Agosti, mwaka huu endapo majadiliano ya
Katiba hiyo hayatajikita kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba.
Hata hivyo, Wassira akijibu kauli hiyo ya Mdee na wabunge wengine
waliopaza sauti kuhusu kukiukwa kwa sheria hiyo alisema: “Kama hamrudi
tutatumia kanuni zile kutafuta akidi na Bunge litaendelea.”
“Tusigeuze Bunge hili kuwa Bunge la Katiba… Bunge la Katiba
lipo tena lipo kisheria…. Kuna watu wanageukageuka wanasema sheria
ilivunjwa, lakini hawasemi kifungu gani kilivunjwa,” alisema Wassira.
Wassira alisema wajumbe wa Bunge la Katiba walitunga Kanuni za Bunge
hilo na miongoni mwa waliokuwa walimu wa kanuni hizo alikuwa Ismail
Jussa na Tundu Lissu ambao ni wajumbe wa Ukawa.
“Kanuni tuliyotunga ambayo haipingani na Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ni Bunge hilo kuwa na mamlaka ya kubadili, kurekebisha, kuboresha
na kadhalika,” alisema Wassira na kuongeza:
“Sasa leo wenzetu baada ya kuamua kutoka wanasema tunavunja sheria
eti kwa sababu tunapingana na mawazo ya wananchi. Hiyo siyo sawa.
Tunapingana na maoni yapi ya wananchi?
Wassira alisema kama ni hoja ya maoni ya wananchi, upande wa Zanzibar
asilimia 60 walitaka Serikali ya mkataba lakini rasimu iliyopo mbele ya
Bunge Maalumu la Katiba haina mapendekezo ya mkataba.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliwasihi wajumbe
wa Ukawa warejee bungeni, akisisitiza kuwa Katiba Mpya itapatikana kwa
maridhiano na si kwa wajumbe kuasi Bunge.
Mabilioni Bunge la Katiba utata
Wabunge wa upinzani wamehoji kiasi cha fedha kilichotumika kugharimia
awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu la Katiba. Kuhoji huko kumetokea
wakati, Wizara ya Katiba na Sheria ikisema Sh21 bilioni zimetengwa kwa
ajili ya awamu ya pili ya Bunge la Katiba linalotarajia kuanza vikao
vyake Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.
Naibu Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa wizara hiyo,
Rashid Ali Abdalla, akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Makadirio ya
Mapato na Matumizi kwa mwaka 2014/15 alisema zipo ndimi mbili kutoka
kwa mawaziri watatu ambazo zinasababisha mkanganyiko wa kiasi
kilichotumika katika Bunge hilo, jambo linalohitaji kuhojiwa na kupata
ukweli.
Abdalla alisema kwa nyakati tofauti, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
amekaririwa akisema Bunge hilo lilitumia Sh27 bilioni kauli iliyoungwa
mkono na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge)
William Lukuvi.
Hata hivyo, alisema utata ulijitokeza baada ya Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk Asha-Rose Migiro kueleza kuwa Bunge la Katiba lilitumia kiasi
cha Sh24.4 bilioni kiasi ambacho kinatofautiana na wenzake.
Mwandosya ataka wimbo mpya
Katika hatua nyingine; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark
Mwandosya ametoa hoja ya kuubadilisha Wimbo wa Taifa ili kulinda
uzalendo Tanzania.
Alitoa hoja hiyo alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya Katiba na
Sheria kwa kueleza kuwa, wimbo unaotumika sasa ni wa kuazima kutoka
Afrika Kusini, hivyo ni kama kuenzi utamaduni wa huko badala ya
kudumisha na kujenga uzalendo kwa Watanzania, hasa vijana.
“Tufikirie kuwa na wimbo wenye hadhi ya Kitanzania ili kuendeleza
uzalendo zaidi na kuachana na huu uliopo. Tunaweza hata tukautumia wimbo
wa ‘Tanzania… Tanzania’ ambao ni wa kwetu tofauti na uliopo ambao
tumeuazima,” alisema Profesa Mwandosya.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Julius Mathias na Habel Chidawali.
0 comments:
Post a Comment