banner

Friday, May 9, 2014

Rais Kikwete awapa rambirambi Wanigeria.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametoa salamu za rambirambi na pole nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Nigeria Mheshimiwa Goodluck Jonathan na wananchi wa Nigeria kufuatia mfululizo wa vitendo vya ugaidi ambavyo vimepoteza maisha ya maelefu ya wananchi wa nchi hiyo na kutekwa nyara kwa mamia ya watu wakiwemo wanafunzi wa kike wa sekondari.

Katika salamu zake za pole kwa Rais Jonathan, Rais Kikwete amesema: “Napenda kutoa salamu za rambirambi na pole zetu nyingi kwako Mheshimiwa Rais na wananchi wa Nigeria kufuatia mfululizo wa vitendo vya kigaidi ambavyo vimepoteza maisha ya maelfu ya wananchi wa nchi hiyo na wengine kutekwa nyara. Tumekuja kuonyesha mshikamano wetu na wananchi wa Nigeria.”

Rais Kikwete ametoa pole hizo mwanzoni mwa hotuba yake kwenye mkutano wa marais uliozungumzia umuhimu wa miundombinu ya kimkakati katika Afrika ikiwa ni sehemu ya Kongamano la Uchumi Duniani (WEF) Afrika kwenye Hoteli ya Transcorp Hilton mjini Abuja, Nigeria.

Akizungumza mbele ya Rais Jonathan na viongozi wengine wa Afrika, Rais Kikwete amemwambia kiongozi huyo wa Nigeria: “Tulishauriwa sana tusije kuhudhuria kongamano hili kwa sababu ya hali ya usalama. Lakini tusingefika tungewapa ushindi magaidi hawa ambao wanasumbua sehemu kubwa ya Bara letu. Mheshimiwa Rais sala zetu ziko nawe na wananchi wa Nigeria katika kipindi hiki kigumu.”

Serikali ya Nigeria imekuwa inapambana na vikundi vya kigaidi na hasa kile cha Boko Haram ambacho kimekuwa kinaendesha kila aina ya ugaidi hasa katika maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo.

Wiki tatu zilizopita, kikundi hicho ambacho lengo lake kuu ni kupinga elimu ya magharibi kiliteka watoto zaidi ya 200 wa kike kutoka mabweni ya shule moja ya sekondari kaskazini mwa nchi hiyo.

Mpaka sasa watoto hao hawajapatikana, jambo ambalo linaipa shinikizo kubwa Serikali ya Nigeria. Boko Haram kimetishia kuwauza sokoni watoto hao wa kike.

Siku mbili zilizopta, kikundi hicho kiliteka nyara watu wengine wanane na usiku wa jana, kimeua watu wanaokadiriwa kufikia 300 katika vijiji mbali mbali vya eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
8 Mei, 2014

Socializer Widget By Blogger Yard
SOCIALIZE IT →
FOLLOW US →
SHARE IT →

0 comments:

Post a Comment