Mzimu wa Bunge la Katiba umeanza kulizunguka bunge
la bajeti, baada ya Mwenyekiti wa kambi ya upinzani bungeni jana, Freeman Mbowe,
kuwasilisha hotuba yake yenye madai mengi kuhusu bunge la katiba.
Mbowe alitoa madai hayo wakati akisoma taarifa ya
kambi ya upizani katika mkutano wa bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015
unaoendelea mjini Dodoma.
Mbowe alidai mchakato wa bunge maalum la katiba
umetawaliwa na CCM na kusema kamwe wajumbe wa bunge hilo kutoka Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA) hawatarudi bungeni kujadili katiba, akisema hawakubali kuwa
sehemu ya wasaliti wa Watanzania.
Alisema umoja huo utarejea kujadili katiba kama tu rasimu ya katiba itaheshimiwa huku wajumbe
wakiheshimiana.
Aidha alidai kati ya wajumbe 201 walioteuliwa
kuunda bunge la katiba, 160 ni wanachama na makada wa CCM.
Kuhusu bajeti ya bunge maalum, alisema
haikuidhinishwa na bunge na wala wabunge hawana taarifa.
Alisema bunge halifahamu chochote kuhusu gharama
zilizotumika na bunge maalum la katiba na halifahamu gharama itakayotumika
katika mkutano ujao wa bunge hilo.
Mbowe aliitaka serikali kuanisha bajeti nzima ya
bunge maaalum, fedha ambazo tayari zimeshatumika, nani alijadili na kupitisha bajeti hiyo na
lini na kwa haraka gani Mkaguzi wa Fedha (CAG) aliidhinisha na kupitisha matumizi
hayo.
Aidha, alivishutumu vyombo vya habari vya umma
(TBC1 na TBC Taifa) na magazeti ya Daily News na Habari Leo kwa kuipendelea CCM
na makada wa chama hicho, wakati vinaendeshwa kwa kodi ya wananchi, huku
akisema hana tatizo na gazeti la Uhuru kwa sababu linamilikiwa na CCM na vyombo
vya habari vya binafsi.
Awali Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema Watanzania
wana kila sababu ya kuutetea Muungano wa Tanzania, kwani ndio wenye hadhi ya utanzania
wao.
Alisema Watanzania wana kila sababu ya kuikubali miaka
50 ya Muungano kwa vile asilimia 90 ya Watanzania wamezaliwa katika mfumo wa muungano
wa serikali mbili na wana kila sababu ya kuulinda na kuutetea.
Alisema kutokana na hali hiyo ndio maana serikali
imeamua kuandaa mchakato wa katiba ambao utaangalia namna ya Watanzania watakavyofaidika
na hazina ya nchi yao.
Alisema serikali ina imani kubwa mchakato huo
utaenda vizuri baada ya awamu ya kwanza kumalizika na kuihakikisha Tanzania katiba
iliyo bora.
Aidha alisema serikali inaendelea na mchakato wa
vitambulisho vya taifa ambao tayari,umeibua changamoto mbali mbali ambazo
serikali inakabiliana nazo.
Alisema shughuli za kiuchumi zimeongezeka na
kufanya pato la taifa kuongezeka huku kukiwa na
mahitaji makubwa ya kijamii kwa kuwa hali ya utegemezi nchini bado ni
kubwa kutokana na kuwapo kwa kiwango kikubwa cha vijana na watoto yatima.
0 comments:
Post a Comment