JESHI la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia mkazi mmoja wa kijiji cha Songambele wilayani Maswa mkoani hapa, kwa tuhuma za kutaka kumuua mtoto wake kwa kumtupa na kumtelekeza nje ya nyumba ili aliwe na fisi. Kamanda wa polisi mkoani Simiyu, Charles Mkumbo alisema ofisini kwake mjini hapa jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa nane za usiku wakati mtuhumiwa Baya Seni (30) akiwa amelala na familia yake kijijini hapo, ndipo alipokurupuka ndani akampiga mtoto wake Amos Baya (3) na kisha kumtupa na kumtelekeza nje ya nyumba. Alisema, Seni katika maelezo yake kituo cha polisi alisema alifikia uamuzi huo kwa kuwa hakuona thamani ya mtoto wa kiume kwenye familia yake kwani uzoefu umeonesha kuwa watoto wa kiume wakikua hudai kupata mirathi kutoka kwa wazazi wao . Alisema kinyume chake watoto wa jinsia ya kike wakikua watamuongezea utajiri wa mifugo atakapolipwa mahari ili waolewe na baada ya kuolewa hawawi mzigo tena kwenye familia yake bali mzigo huo huhamia kwenye familia atakayoolewa. Mtoto huyo aliokolewa na majirani baada ya kusikia kilio. Mama wa mtoto huyo Elizabeth Paulo alisema, mume wake alikuwa akimtesa sana mtoto wake akimbagua kwa vile yeye ni wa jinsia ya kiume na kwamba hana faida kwake.
0 comments:
Post a Comment