Serikali imetakiwa kuandaa taratibu za mpito za kushughulikia Uchaguzi Mkuu ujao ili kunusuru nchi kuingia katika mtanziko unaoweza kuwa chanzo cha machafuko ya kisiasa, endapo utafanyika bila kupatikana kwa Katiba Mpya la sivyo Kambi Rasmi ya upinzani haitashiriki.
Hayo yalielezwa jana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alipokuwa akitoa hotuba ya kambi hiyo bungeni kuhusu Makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Hatuwezi kuingia uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa kwa utaratibu uliopo leo, hatuwezi kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani na Tume ya Uchaguzi kama ilivyo leo, hatuwezi tena kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani wakati matokeo ya uchaguzi wa Rais hayawezi kuhojiwa mahakamani.”
Aliongeza: “Hatuwezi kuingia kabla na hoja ya mgombea huru haijapatiwa majibu, tukiwa na daftari la wapigakura lililopo leo na hatuwezi kulikubali daftari jipya litakalotengenezwa kama wadau wote hatutashirikishwa kikamilifu.”
Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku moja tu baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwasilisha bungeni, Bajeti ya ofisi yake ambayo imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Mbowe alisema kama ilivyo kawaida, Serikali na CCM inaweza kupuuza tahadhari hizo na kulazimisha kwenda katika chaguzi hizo katika mazingira ambayo hayana mwafaka kama inavyoonekana sasa katika Mchakato wa Katiba Mpya.
Ukawa haitarejea bungeni
Katika hotuba hiyo iliyobezwa na wachangiaji wa CCM kuwa imezungumzia Katiba badala ya Bajeti, Mbowe alisema wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hawatarejea katika Bunge la Katiba mpaka watakapohakikisha kuwa maana halisi ya uwepo wa Bunge hilo unafuatwa.
Alisema kama lengo ni kutumia mwavuli wa Bunge Maalumu la Katiba ili kuendeleza mfumo wa kikatiba na muundo wa muungano uliopo sasa, wajumbe wa Ukawa hawatakuwa sehemu ya usaliti huo kwa Watanzania.
“Kama kitakachojadiliwa katika Bunge la Katiba kitalenga kuboresha matakwa ya wananchi kama yalivyodhihirishwa katika Rasimu ya Katiba na taarifa za tume, wanachama wa Ukawa watakuwa tayari kurudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba ili kuendelea na mjadala wa rasimu,” alisema Mbowe.
Ofisi ya Rais
Mbowe alisema kati ya wajumbe 201 wa Bunge la Katiba walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, zaidi ya wajumbe 160 ni wanachama wa CCM.
Alisema hofu ya Kambi ya Upinzani kwamba CCM ingetumia mamlaka ya Rais katika uteuzi wa wajumbe wa bunge hilo, sasa imedhihirika wazi.
Alisema wajumbe hao walichomekwa kwenye Bunge Maalumu kwa kutumia kivuli cha waganga wa jadi, taasisi za kidini, asasi za kiraia, taasisi za kitaaluma na watu wenye malengo yanayofanana.
“Hatua hii imechangia kujenga mazingira ya kutokuaminiana na hivyo kuweka msingi mbaya wa mchakato husika,” alisema.
Alisema hata lilipoanza Bunge la Katiba, CCM iliendelea kufanya hila za kuchakachua kanuni za Bunge la Katiba ili kupitisha hoja zao kirahisi.
“Walipoona wamekwama walimtumia Mwenyekiti wao Taifa (Rais Kikwete) ambaye alitumia kivuli cha urais kusisitiza msimamo wa CCM na kutisha wajumbe wa Bunge la Katiba kwamba kama ukipita muundo wa serikali tatu jeshi litapindua Serikali,” alisema Mbowe.
Alisema Rais Kikwete ndiye aliyebariki uandikaji wa Katiba Mpya Desemba 2010, lakini hivi sasa anaongoza mawaziri wake, viongozi waandamizi, wabunge na wajumbe wa CCM kujadili Rasimu ya Katiba kwa kutukana, kudharau, kubeza, kuzomea na kushutumiana.
Alisema kitendo hicho kinathibitisha kauli zilizowahi kutolewa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kwamba Serikali ya CCM haioni haja ya kuwa na Katiba Mpya kwani iliyopo sasa inatosha
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment