BAADA ya kuwepo malalamiko ya
wasichana wadogo wa nchini kusafirishwa kwenda China kutumikishwa katika
biashara ya ngono pamoja na dawa za kulevya, sasa serikali imenasa
mtandao huo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe alitoa taarifa hiyo juzi bungeni wakati akihitimisha
michango kuhusu bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2014/15 iliyopitishwa.
Chikawe ambaye hata hivyo
hakufafanua kwa undani wa mtandao huo ulivyokamatwa, alieleza Bunge
namna watoto hao wanavyopatikana kabla ya kufikishwa nchi hiyo ya nje.
Kwa mujibu wa Waziri, watu hao
wamekuwa wakichukua watoto wadogo na kuwaambia kwamba wanawapeleka China
hususani mji wa Guanzhou kuwaajiri kwenye saluni na maduka.
Alisema kinara wa usafirishaji
amekuwa akitambuliwa kwa jina la ‘Mama’ ambaye baada ya kufika nchini
humo, huwanyang’anya watoto hao hati zao za kusafiria. Imebainika zipo
hata wakala zinazojihusisha na biashara hiyo haramu ya binadamu.
“Wakifika, Mama anawanyang’anya
pasipoti zao. Anawaambia ili kuwarudishia, lazima watimize masharti ya
kumpa kati ya dola 8,000 na 10,000 baada ya kutumika katika vitendo vya
ngono,” alisema Waziri Chikawe.
Aliendelea kueleza kuwa
wanaposhindwa kutimiza masharti hayo, hukutana na Wanigeria ambao huwapa
hati bandia za kusafiria na kisha kuwaingiza katika biashara ya
kusafirisha dawa za kulevya kwenda nchi mbalimbali.
“Tumenasa mtandao huu…polisi
imenasa mtandao,” alisema Waziri na kutoa mfano kwamba hivi karibuni,
alikamatwa mtu akiwa na hati ya kusafiria akimpelekea binti mmoja.
Alisema binti huyo alipoulizwa juu ya hati hiyo, alikuwa hafahamu
anakokwenda.
Awali, taarifa juu ya kuwepo
usafirishaji wa wasichana wadogo kwenda China kwa ajili ya kutumikishwa
katika ngono, ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe baada ya kutoka ziarani nchini humo.
Membe alisema serikali
inashirikiana na ubalozi wa China katika kubaini wahusika wa biashara
hiyo sanjari na mkakati wa kuhakikisha wasichana hao wanarudishwa
nchini.
Akielezea mikakati ya serikali
katika kukabili biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, Waziri
Chikawe alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014 Sekretarieti ya
kupambana na biashara hiyo imeratibu vikao vinne vya Kamati ya kupambana
nayo.
Aidha imeandaa kitabu cha anuani na
majina ya watoa huduma kwa waathirika wa biashara haramu ya
usafirishaji binadamu na vilevile kutengeneza rasimu ya kanuni za sheria
ya kupambana na biashara hiyo nchini.
Katika mwaka wa fedha 2014/2015
sekretarieti itakamilisha kutengeneza kanuni za Sheria ya kupambana na
biashara hiyo ya mwaka 2008. Pia itatoa elimu na kuimarisha mikakati ya
kupambana na biashara hiyo ya kusafirisha binadamu.
Watanzania zaidi ya 100 wakiwemo
wasichana 20 wamedaiwa wapo gerezani nchini China wakijihusisha na
biashara ya dawa za kulevya.
0 comments:
Post a Comment