MKAZI wa wilaya ya Urambo mkoani Tabora,
Mwamini Adamu ametolewa mfuko wa kizazi na kukatwa sehemu ya utumbo
baada ya mganga wa idara ya upasuaji katika wilaya hiyo kusahau kitambaa
tumboni kwa mwanamama huyo wakati akijifungua.
Kutokana na kumsababishia ulemavu huo kwa uzembe, Mwamini
ameifikisha Halmashauri ya wilaya ya Urambo kwenye Mahakama Kuu Kanda ya
Magharibi akidai fidia ya Sh milioni 500.
Mwamini ambaye anadai kuwa alipwe kiasi hicho cha fedha kutokana na
uzembe wa uliofanywa na Dk Jacob Kamanda aliyemfanyia upasuaji wakati
wa kujifungua na kumsababishia aondolewe mfuko wa kizazi pamoja na
kukatwa utumbo.
Mwamini pamoja na mumewe Idrisa Jafari katika madai yao wametaka
walipwe fedha hizo kutokana na makosa ya uzembe uliofanywa na wataalamu
wa upasuaji kwa kuacha kitambaa tumboni mwa mama huyo.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Amir Mruma jana, mama huyo
alidai kuwa Januari 6 mwaka 2011 alijifungua kwa upasuaji baada ya hapo
hali yake ilizidi kuwa mbaya huku akitokwa usaha ukeni na sehemu ya
tumbo kwenye mshono.
Huku akiongozwa na wakili wa kujitegemea Mussa Kwikima, mama huyo
aliiambia mahakama kuwa hali hiyo ilifanya apelekwe hospitali ya mkoa wa
Tabora Kitete bila mafanikio ndipo ikamlazimu kwenda Itigi kwa matibabu
zaidi.
Katika uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na madaktari bingwa, Haile
Sales ambaye ni raia wa Italia pamoja na Anatole Lukonge wa hospitali
hiyo ya Itigi, waligundua kuwa kuna kitu tumboni kama uvimbe hivyo
wakalazimika kumfanyia upasuaji mwingine.
Baada ya upasuaji huo walikuta kitambaa cha rangi ya kijani ambacho
kilikuwa kimeozesha mfuko wa uzazi pamoja na utumbo kugandana na
kitambaa hicho ikabidi kitambaa hicho kutolewa na kusababisha kupasuka
kwa utumbo ili kumnusuru maisha yake.
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya akinamama na ambaye ni mganga
mkuu wa hospitali ya Itigi, Anatory Lukonge katika ushahidi wake
ameiambia mahakama hiyo kuwa alimpokea mlalamikaji akiwa anatokwa na
usaha ukeni na sehemu iliyoshonwa.
Alisema wakati walipojaribu kukiondoa kitambaa hicho kibofu cha
mkojo kilipasuka wakalazimika kumuwekea mpira ili uweze kumsaidia
kutolea uchafu.
Kesi hiyo ya madai namba 13/2011 imeahirishwa hadi Agosti tatu
mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa kwa upande wa utetezi kuleta
mashahidi wake.
Chanzo: Habari leo
0 comments:
Post a Comment