Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo akizungumza wa mkutano na waandishi Dar es Salaam jana. Picha na Salhim shao.
Wakati kukiwa na utata wa kifo cha Meneja wa Biashara ya Petroli wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imebainika kuwa tofauti
ya takwimu kati ya mamlaka hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
iliyotolewa kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti ni Sh25 bilioni.
Meneja huyo, Julius Gashaza alikuwa akihudhuria kikao kilichokuwa
kikijadili tofauti hiyo bungeni Dodoma na baadaye aliporudi Dar es
Salaam akakutwa amejinyonga hotelini huku ikielezwa kuwa alirudi akiwa
amejawa hofu na kukosa amani.
Vyanzo vyetu ndani ya kamati hiyo vimeeleza kuwa tofauti
iliyobainika katika hesabu za taasisi hizo za Serikali ni lita
11,755,161, ambazo zingeuzwa kwa bei ya sasa ya petroli mkoani Dar es
Salaam ya Sh2,200 zingepatikana Sh25.86 bilioni.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, takwimu za TRA zinaonyesha kuwa kati ya
Julai 2013 hadi Machi mwaka huu, kiasi cha mafuta kilichoingizwa nchini
kilikuwa lita 2,189,240,000 wakati Ewura ilionyesha ni lita
2,177,484,839.
Hata hivyo, baada ya utata huo na Kamati ya Bajeti chini ya Andrew
Chenge kuitaka Serikali itoe ufafanuzi wa tofauti hizo, Serikali
iliwasilisha taarifa yake Jumapili ikisema takwimu zote ni sawa.
Katika ufafanuzi wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
alisema uhakiki wa takwimu hizo ulibaini kuwa zote zilikuwa ‘sahihi’ na
kwamba tofauti iliyopo inatokana na upimaji wa mafuta.
Nchemba alikaririwa akisema TRA hupima mafuta kwenye meli mara
inapoingia na kukadiria kodi wakati Ewura hupima mafuta yanapopokelewa
kwenye matanki.
“Kwa kuwa wakati mwingine meli hutumia muda mrefu tangu zinapoingia
hadi zinapoteremsha mafuta, sehemu ya mafuta ambayo TRA huhesabu kama
yameingizwa katika mwezi mmoja wakati Ewura hupata takwimu za kiasi cha
baadhi ya mafuta hayo katika mwezi unaofuata na hiyo ndiyo
iliyosababisha kuwapo kwa tofauti hiyo ambayo hata hivyo ni ndogo.”
Kulingana na takwimu hizo, kiasi cha mafuta kilichoonyeshwa na TRA
kilikuwa juu kuliko kile kilichoonyeshwa na Ewura na haijajulikana iwapo
kutofautiana huko kwa takwimu kuliifanya Serikali kumweka kitimoto
Gashaza.
Alikuwa na hofu
Sintofahamu imeendelea kugubika kifo cha Gashaza na sasa imeelezwa
kuwa alirudi kutoka Dodoma akiwa amejawa hofu na kukosa amani.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema jana kuwa ingawa
hakuzungumza na Gashaza baada ya kurudi kutoka Dodoma, taarifa za
polisi na kutoka kwa mkewe zinaeleza kuwa alirudi akiwa na hofu na ndiyo
sababu ya kuondoka nyumbani kwake na kwenda kulala hotelini.
“Tumepata mshtuko mkubwa kuhusu msiba huu. Ndiyo maana tunataka
kujua alikuwa na hofu ya nini na kwa nini. Kama alitishiwa maisha ni
watu gani walimtishia maisha. Ndiyo majibu tunayoyataka kutoka kwa
wanausalama,” alisema Ngamlagosi.
Mkurugenzi huyo alisema si kweli kuwa marehemu Gashaza alikwenda
bungeni kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti, bali alikwenda kuhudhuria
mkutano wa kawaida ambao haukuwa ukihusisha Ewura na tuhuma zozote.
“Gashaza alikwenda kuniwakilisha, hakwenda kwa minajili ya
kuhojiwa, Ewura iliitwa kushiriki mkutano wa kawaida, ambao ni miongoni
mwa taratibu za kawaida za kazi,” alisema.
Ngamlagosi alisema kifo cha Gashaza bado ni kitendawili kikubwa
ambacho kinaweza kufumbuliwa na watu wa usalama pekee, kwa kuwa meneja
huyo alikuwa mwadilifu na tegemeo kubwa kwa mamlaka hiyo.
“Tunamfahamu kama mtu ambaye si mwepesi kurubuniwa kwa lolote lile,
hakuwahi kukumbwa na kashfa yoyote ile tangu aanze kazi hapa mwaka
2007,” alisema na kuongeza:
“Ameleta mabadiliko makubwa kwenye mamlaka. Mpaka sasa hatujui nini au nani amemkwaza.”
Alisema Gashaza alikuwa mwadilifu kwa kiasi kikubwa licha ya kuwa
alikuwa akifanya kazi kwenye kitengo nyeti cha ukaguzi wa mafuta ambako
majukumu yake makuu yalikuwa ni kuangalia ubora, miundombinu, biashara,
bei na ununuzi wa mafuta, kusimamia uingizwaji wa mafuta nchini, utoaji
wa leseni na kuangalia jinsi wafanyabiashara wanavyofanya kazi.
Mhudumu wa gesti
Mhudumu wa gesti ya Mwanga Lodge ambayo Gashanza alipanga kabla ya
mauti kumkuta, Ngina Riwa alisema mteja wake huyo alifika Jumamosi saa
3:00 usiku na kupanga chumba namba 113.
Alisema baada ya muda mfupi walifika watu watatu, wanawake wawili
na mwanamume mmoja na kuonana na mteja wao na baada ya kushauriana
kidogo wakaingia naye chumbani.
“Huko chumbani hawakukaa sana na haikuzidi hata nusu saa na baadaye
yule mteja akatoka nao kuwasindikiza. Hakufika mbali, akarudi tena na
kuingia chumbani.
Riwa alisema wakati mteja wake anaingia chumbani kulala ilikuwa takribani saa nne usiku na hakutoka tena.
Alibainisha kuwa asubuhi kati ya saa 12:30 na 1:00 asubuhi alikuja
tena yule rafiki yake mwanamume kumulizia mteja wake kama alikuwa
ameamka.
“Alikwenda kumgongea lakini hakufungua, akarudi kwangu tukaenda
naye tukagonga hakufungua, ndipo tukashirikiana na mlinzi kufungua
dirisha kwa nje na kumwona akiwa amelala chini.
“Tukawapigia simu polisi kutoka Kituo cha Ali Mboa ambao
hawakuchukua muda wakaja. Baadaye wakaja polisi wenye vyeo vya juu
wakapimapima wakaondoka na mlinzi na bosi wetu kama saa tatu asubuhi
hivi,” alisema mhudumu huyo.
Uchunguzi wa polisi
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engbert Kiondo alisema
uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho unaendelea kwa kuangalia maeneo
matatu.
Alisema utajielekeza kubaini kama kulikuwa na mgogoro wowote wa
kifamilia au iwapo alikuwa na tatizo lolote kazini kwake kabla ya kifo
chake na mazingira kilipotokea kifo hicho na baada ya kujiridhisha
watatoa taarifa kamili kwa vyombo vya habari.
“Kuna maswali mengi ya kujiuliza kwa nini hakutaka kulala nyumbani
kwake usiku ule badala yake akaamua kulala hotelini, tunafanya upelelezi
kubaini nini hasa kilimsukuma kujinyonga,” alisema.
Alisema pia wanasubiri ripoti ya uchunguzi ya daktari ambayo wataitumia katika upelelezi wao kubaini chanzo.
Alisema polisi watachunguza kama Gashaza alijinyonga kweli au aliuawa na kutengenezewa mazingira ya kujinyonga.
Ampigia simu rafiki yake
Kiondo alisema Gashaza alipofika katika nyumba ya kulala wageni,
alimpigia simu rafiki yake wa karibu anayeitwa Sibitwango na kumweleza
kuwa mambo yamekuwa magumu na hakujisikia vizuri.
Usiku huo, Kiondo alisema Sibitwango pamoja na mke wa marehemu
Judith walimfuata katika hoteli aliyofikia na kumsihi arudi nyumbani
akapumzike lakini yeye (Gashaza) alisisitiza kulala hapo kwa sababu
tayari alikuwa ameshalipia chumba hicho.
Kiondo alieleza kuwa siku iliyofuata Sibitwango mwenyewe ndiye aliyetoa taarifa polisi na kueleza mazungumzo yao kabla ya kifo.
Utata bungeni
Wakati inaelezwa kuwa kulikuwa na tofauti ya takwimu kati ya zile
za TRA na Ewura kuhusu kiwango cha mafuta kilichoingia kwenye soko,
taarifa zaidi zimeeleza kuwa katika kikao cha Kamati ya Bajeti, Gashaza
hakuulizwa swali hata moja.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema marehemu hakuhojiwa labda
kilichomfanya ajiue ni hofu iliyotokana na mahojiano baina ya kamati
hiyo na watendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Alisema kamati hiyo iliwaita viongozi wa Wizara ya Fedha na Wizara
ya Nishati na Madini ili kuwahoji kwa nini Sh50 zilizoongezwa katika
mafuta ya petroli na dizeli hazikwenda Rea?
Mjumbe huyo alisema kati ya zaidi ya Sh100 bilioni zilizotakiwa
kwenda Rea ni Sh17 bilioni tu zilizopelekwa na fedha nyingine
zilielekezwa kwenye matumizi mengine ambayo hayakuidhinishwa na Bunge.
Credit:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment