banner

Wednesday, May 14, 2014

Baraza kivuli la UKAWA halina mashiko kisiasa




KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Alikael Mbowe ametangaza baraza lake kivuli, kufuatia ahadi yake ya hivi karibuni kuwa atalivunja lile la awali, lililokuwa likiundwa na wabunge kutoka Chadema pekee, ili sasa awajumuishe na wabunge wa vyama vingine vya siasa kutoka upinzani.

Baraza hilo jipya limetangazwa likiwa na mawaziri vivuli kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na hivyo kutimiza ahadi hiyo ambayo kimsingi imetokana na muungano wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba linalounda umoja unaojulikana kama Ukawa ambao walisusia vikao vyake hivi karibuni.

Ingawa tukio hili linaonekana kama ni jambo jema kwa wapinzani, hasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao, lakini kwa wanaopenda kujikumbusha na kutafakari watabaini kwamba tukio hili haliko katika uhalisia wake, bali linatokana na msukumo wa kisiasa zaidi.

Wengi bado tunakumbuka jinsi bunge hili lilipoanza mwaka 2010 tuliposhuhudia maneno ya kashfa, kejeli, vijembe na mambo chungu mzima baada ya Mbowe kutangaza rasmi kwamba baraza lake la mawaziri vivuli, litaundwa na wabunge wa chama chake pekee, akifuta utaratibu ambao ulifuatwa na CUF, wakati ule wakiwa chama chenye wabunge wengi wapinzani bungeni.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni chini ya CUF, iliongozwa na Hamad Rashid huku Dk. Wilbroad Slaa akiwa Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni. Chadema, wakati wakikataa kushirikisha vyama vingine katika baraza hilo, ilidai kwamba CUF walikuwa ni CCM B, wakirejea Serikali ya Umoja wa Kitaifa kule Zanzibar.

Baada ya kauli hiyo, yalifuata maneno mengi kiasi kwamba hadi shughuli za Bunge zilipoanza na kuendelea, kila chama kilishuhudia majeraha mengi ambayo hayawezi kuwa yamepona, mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Kama kweli Mbowe na Chadema waliamini katika ushirikiano na vyama vingine ili kuidhoofisha CCM, umoja huu ulipaswa kuwepo wakati ule, kwa sababu hakuna jambo lolote ambalo limebadilika, miaka minne tokea Bunge hili lianze.

Kinachoonekana, ni muungano wenye masilahi kwa vyama vya Chadema na CUF, ambavyo kimsingi, vinajiandaa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu 2015. Kwa nini muungano huu uwe sasa? Jibu ni rahisi, kila chama kina masilahi kwenye mchakato wa katiba mpya ya nchi na hivyo umoja wao ni wenye kulenga mahitaji yao binafsi.

Chadema ni chama chenye nguvu Bara na CUF kule Zanzibar. Hawa wote wanajua endapo katiba mpya itaandikwa kwa jinsi wanavyotaka wao, ni rahisi kwao kushika dola, Bara kwa Chadema na Visiwani kwa CUF.

Ikumbukwe pia kuwa watu hawa wametangaza nia yao ya kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi mkuu wa mwakani. Nina shaka na utekelezaji wa suala hili kutokana na hulka ya kila chama kutaka ukubwa hivyo upo uwezekano mkubwa wa vyama hivi kukinzana katika hatua ya mwisho kwa sababu kama nilivyosema mwanzo, simuoni aliye tayari kuwa mdogo!

Socializer Widget By Blogger Yard
SOCIALIZE IT →
FOLLOW US →
SHARE IT →

0 comments:

Post a Comment