Jeshi la polisi mkoani Arusha limefanikiwa kukamata
bunduki tatu za kivita zilizokuwa zikitumiwa na wananchi wa kabila la Wasonjo
na Wamasai kinyume cha sheria, wilayani Ngorongoro katika mapigano mbalimbali
yaliyosababisha vifo na majeruhi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda
wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alitaja silaha hizo kuwa ni SAR yenye namba 20034823 ikiwa na risasi
saba, SMG yenye namba NH-4200 ikiwa na magazine yenye risasi tano na G3 yenye
namba D60365 ikiwa na magazine yenye risasi tano.
Kamanda Sabas alisema kukamatwa kwa silaha hizo
kumetokana operesheni kambambe ya jeshi hilo kwa kushirikiana na wazee wa ukoo
wa makabila mawili ya Wasonjo na Wamasai katika vijiji vya Olorien na Mgongo, wilayani
humo.
Alisema operesheni hiyo imekuja kufuatia mapigano ya
mara kwa mara ya kulipiza kisasi baina ya makabila hayo, ambapo watu wa kabila la
Wasonjo mnamo Aprili 8 mwaka huu
walivamia gari aina ya Landrover linalodaiwa kumilikiwa na Wamasai na
kulishambulia kwa risasi.
Aliongeza kuwa tukio hilo lilisababisha vifo vya watu wawili
akiwemo mwanafunzi wa kidato cha tatu na kuwajeruhi wengine saba wakitoka kwenye
vijiji vinavyokaliwa na Wasonjo.
Alisema tukio hilo
lililenga kulipiza kisasi kwani kabla ya tukio hilo mtu mmoja wa kabila la kimasai aliuawa
wakati akitokea katika kijiji cha Olorieni.
Alisema baada ya mapigano hayo ambayo yamekuwa
yakijitokeza mara kwa mara wilayani humo, jeshi la polisi kwa kushirikiana na timu ya wazee wa kimila
kutoka makabila yote mawili waliunda tume ya usuluhishi na kufanikiwa
kupatikana silaha hizo.
Alisema timu hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kurejesha hali ya amani katika vijiji hivyo kwani baadhi ya wananchi walikubali
kusalimisha silaha zao walizokuwa wakitumia katika mapigano mbalimbali ya makabila hayo mawili.
0 comments:
Post a Comment