MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Itiji, jijini Mbeya kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Ezekiel King (52) na mwenzake Bw. Antony Simon (53) wamehukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la shambulio la kumdhuru mwili Bw. Nicholaus Mwakasinga (56), mkazi wa mtaa huo.
Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Maria Batulaine, ambapo Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Bi. Juliana William alisema kuwa, washtakiwa hao walimshambulia na kumjeruhi Bw. Mwakasinga.
"Washtakiwa walimjeruhi kichwani na mkononi katika kilabu cha pombe za kienyeji Mtaa wa Itiji," alisema.
Kutokana na maelezo hayo, mahakama hiyo iliwatia hatiani ambapo Hakimu Batulaine alitoa hukumu hiyo na kuwaambia wanayo fursa ya kukata rufaa kama hawajaridhika na hukumu ambayo imezingatia kanuni ya adhabu namba 225, sura ya 6 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hakimu Batulaine alisema maelezo ya shahidi namba moja, mbili na tatu, yalifanana lakini maelezo ya mashahidi upande wa utetezi yalijichanganya na kuonesha mashaka.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mlalamikaji Bw. Mwakasinga alipigwa, kujeruhiwa na washtakiwa ambao baadaye walimchukua na kumpeleka Kituo cha Polisi wakidai alikuwa akifanya vurugu kilabuni.
Hata hivyo, mlalamikaji baada ya kupata kipigo hicho alilazwa katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo, wodi ya wagonjwa wa akili ili kumpima kama alifanya vurugu kutokana na ugonjwa huo lakini alipotoka, alifungua mashtaka ya kupigwa ambapo washtakiwa walikamatwa na kufunguliwa kesi.
Katika utetezi wake kabla ya kutolewa hukumu Bw. King aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ana watoto sita ambao wanamtegemea.
0 comments:
Post a Comment