Taarifa zinasema kuwa ajali iliyotokea jana katika kijiji cha Yitwimila A, kata ya Kiloleli wilayani Busega katika mkoa wa Simiyu imesababisha vifo vya watu 20 na kuacha takribani watu 40 wakiwa na majeraha, baada ya basi la Luhuye Express lililokuwa likisafiri kutoka katika mji wa Sirari, Tarime mkoani Mara likielekea Mwanza kuacha njia na kugonga nyumba kisha kupinduka.
Dereva wa basi hilo ameripotiwa kutoroka wakati majeruhi walipelekwa katika hospitali za Wilaya na ile ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishina Mwandamizi wa Polisi (SACP), Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema basi hilo liliigonga nyumba ya marehemu, Mwalimu Lazaro Mbofu na kuibomoa yote na kisha kupinduka.
“Hadi sasa kuna maiti 10 walizopatikana katika eneo la tukio, na zaidi ya watu 30 wamejeruhiwa na kukimbizwa Bugando kwa ajili ya matibabu. Ila taarifa kamili nitaitoa baadaye juu ya watu waliokufa na waliojeruhiwa, kwa sasa nimetuma askari wa usalama barabarani kufuatilia,” alinukuliwa Mkumbo akisema.
Taarifa kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti zinasema abiria waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni wanawake 5 na wanaume 7.
Nao walioshuhudia ajali hiyo wamesema basi hilo likiwa katika mwendo mkali, lilianza kuyumba kabla ya kugonga nyumba iliyotajwa hapo juu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Dk Athuman Pembe amesema amepokea majeruhi 60 pamoja na maiti kumi na mmoja. Amesema kati ya majeruhi hao, 25 hali zao siyo nzuri na wamepelekwa katika hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza, na hali za majeruhi waliobaki katika hospitali hiyo zinaendelea vizuri na tayari wengine wameanza kuruhusiwa.
0 comments:
Post a Comment