banner

Wednesday, May 7, 2014

Vurugu kubwa Kibaigwa mkoani Dodoma.....Gari la mbunge lapigwa mawe, Maduka yavunjwa...Gari la Polisi nalo lavunjwa vioo, Watu 34 wakamatwa


Na Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu 34 wakazi wa Mji mdogo wa Kibaigwa Kata ya Kibaigwa Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma kwa makosa ya kufanya fujo na kuharibu mali tukio lililotokea tarehe 05/05/2014 majira ya saa 13:30Hrs.

Kamanada wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema Vijana wanaokadiriwa kuwa zaidi ya miatatu wakishirikiana na Wabeba mizigo wa Soko Kuu la Mazao la Kibaigwa, walifanya maandamano bila kibali na kung’oa bango la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa lenya tangazo la kutoruhusu wafanyabiashara kuingiza mazao sokoni bila kulipa ushuru uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

Viwango vya ushuru vinavyotozwa vilipanda tangu tarehe 01.07.2013 ambapo gunia la Kg. 100 za karanga zilipanda kutoka Tshs. 1000/= hadi Tshs 3000/=, guina la mahindi lilipanda kutoka Tshs. 500/= hadi Tshs. 1000/=, dumu la mafuta ya alizeti lilianza kutozwa Tshs. 500/=, gunia la mashudu lilianza kutozwa Tshs. 1000/=, gunia la alizeti lilianza kutozwa Tshs. 1000/= ushuru ambao unapingwa na wabeba mizigo.

Vijana  hao wabeba mizigo walifanya fujo kwa kufunga barabara kuu ya Dodoma – Morogoro kwa mawe na kuchoma mataili, pia walivamia maduka na bar za jirani na kupora vinywaji na kuvunja majokofu.

Kamanda MISIME amesema katika vurugu hizo walisababisha uhalibifu wa mali kwa kushambulia magari kwa mawe likiwemo gari la Mbunge wa Tanga Mh. OMARI NUNDU lenye namba za usajili T.419 CWC Land Cruiser Prado ambaye aliyekuwa akienda Bungeni Dodoma, pia gari la Polisi namba PT. 0960 Land Rover lilivunjwa kioo cha mlango wa mbele kulia na basi la Kampuni ya Shabaha lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam lilivunjwa kioo cha mbele.

Kamanda MISIME amesema chanzo cha vurugu hizo ni wabeba mizigo wa soko la mazao kibaigwa kupinga kitendo cha Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuweka tangazo la kutoza ushuru wa mazao sokoni hapo wakidai kwamba linawakosesha kufanya kazi zao kwani wateja wanashindwa kuingiza mazao sokoni na wao kukosa kazi.

Socializer Widget By Blogger Yard
SOCIALIZE IT →
FOLLOW US →
SHARE IT →

0 comments:

Post a Comment