USHIRIKA wa wachungaji wa Kipentekoste nchini (PPFT) umemtaka
Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Askofu
Zakaria Kakobe, kuacha tabia ya kutumia mwavuli wa dini kuhubiri chuki
na uchochezi kwa wananchi.
Akizungumza juzi wakati wa kufunga semina ya viongozi wa dini wa
Mkoa wa Kilimanjaro iliyofanyika katika ukumbi wa Umoja Hostel,
Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji nchini, Askofu Ikongo alisema kauli
za Askofu Kakobe zimekuwa za hatari na zinaweza kuliingiza Taifa kwenye
machafuko ya kidini.
“Nchi yetu imekuwa na
dalili za viashiria vya kutoweka kwa amani na utulivu, kutokana na
baadhi ya viongozi wa dini kujiingiza kwenye siasa na kuanza kutoa kauli
za kuashiria uchochezi na kupandikiza chuki kwa waumini…sasa umefika
wakati sisi viongozi wa dini hatuwezi kunyamaza kwani tutaonekana na
matamko yanayotolewa kiholela kwa kutumia mwamvuli wa upentekoste,” alisema Askofu Ikongo.
Alisema Askofu Kakobe amekiuka uadilifu wake, kwani Aprili 20 mwaka
huu katika kanisa lake la Mwenge, alitoa kauli kuwa atapambana hadi
Tanganyika irudi hata kwa kukatwa kichwa, kauli ambayo inadhihirisha
ugaidi.
Askofu Ikongo alisema kauli kama hiyo haistahili kutolewa na
mtumishi yeyote wa Mungu, kwani mtu mwenye uwezo wa kusema hata akatwe
kichwa sio wa kawaida bali ni mtu aliye na mafunzo ya kujitoa mhanga
kama gaidi.
“Tunasikitishwa na kauli za
Askofu Kakobe ambazo zinaweza kuliletea Taifa machafuko ya kidini…siku
ya Pasaka Aprili 20 mwaka huu aligeuza mimbari kuwa jukwaa la siasa, kwa
kuhubiri uchochezi kwa kudai; kila mtu anayepigania kurudi kwa
Tanganyika, ana Mungu ndani yake,” alisema.
Kwa mujibu wa Askofu Ikongo, kauli hizo za Kakobe ni za kigaidi na
zina nia ya kuvuruga amani ya Watanzania na kuliingiza taifa kwenye
machafuko, ambayo yataharibu tunu iliyoachwa na Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere.
Alisema ni vyema viongozi wa dini wajikumbushe wajibu wao wa
kuliombea Taifa, na kuwaongoza waumini wao kufuata yaliyo mema badala ya
kugeuka sehemu ya kutumiwa na wanasiasa.
Akifunga semina hiyo Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Grace Makiluli aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Leonidas Gama, alisema
inasikitisha kuona viongozi wa dini kutumiwa na wanasiasa, kwa kutoa
kauli zinazowafanya wananchi kuhoji kama viongozi hao hawatumii dini
kutekeleza malengo ambayo sio mema.
Alisema Serikali bado ina imani na viongozi wa dini, kwa wale
wanaozingatia maadili na utume wao wa kuhakikisha amani iliyodumu kwa
miaka mingi inadumishwa.
Aliwataka waumini kutowaunga mkono wanaotumia mimbari kuwa jukwaa
la siasa kwa kutoa maneno makali yanayohatarisha amani na kupandikiza
chuki miongoni mwa waumini na wananchi.
0 comments:
Post a Comment