NA MOHAMMED ISSA,
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye, amesema kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ni
kundi hatari linaloeneza chuki na kusambaza uongo kwa wananchi.Amelifananisha kundi hilo na Boko Haramu na kwamba tofauti yake ni kwamba UKAWA linatumia silaha ya kusambaza chuki, fitina kwa lengo la kuwagawa Watanzania wazalendo.
Nape alisema silaha zinazotumiwa na UKAWA ni kali zaidi kuliko za Boko Haramu ambao wanatumia silaha za moto.
Alisema silaha ya kueneza sumu na uongo katika jamii ni mbaya zaidi kuliko silaha za moto.
Nape alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani hapa mkoani Tabora.
Alisema sumu ya uongo na unafiki inayoenezwa na UKAWA ni hatari kuliko silaha yoyote na kwamba lengo la kundi hilo ni kuwagawa wananchi wazalendo.
Nape alisema sumu hiyo walianza kuieneza wakati wakiwa bungeni, ambapo walifikia hatua ya kumtukana muasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Hawa jamaa hawana tofauti na Boko Haramu, wanapita kila sehemu kueneza sumu na chuki kwa wananchi, ninawaombeni wakija muwapuuze,”alisema.
Kwa upande wake, mbunge wa Jimbo la Sikonge, Said Nkumba, alisema mtaji wa wapinzani ni kupinga kila kitu kinachofanywa na Serikali ya CCM.
Alisema viongozi wa upinzani wanazunguka kila sehemu kusambaza uongo badala ya kuwapelekea wananchi maendeleo.
“Wapinzani wote wanaokuja Sikonge kazi yao ni kusema bila kuacha hata mfuko wa saruji sasa sijui hayo maneno yao yanaleta faida kwa wananchi,” alihoji mbunge huyo.
Aliwataka wananchi kuwapuuza wapinzani wanotumia muda mwingi kupiga porojo bila ya kufanya mambo ya maendeleo kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, jana ulipokelewa na mamia ya wananchi wa wilaya ya Urambo, wakiwemo madiwani wawili wa Chama cha CUF.
Kinana ambaye amefuatana na Nape waliwasili Urambo na kupokewa na
mbunge wa jimbo hilo, Samuel Sitta, na viongozi wengine wa Chama.
0 comments:
Post a Comment