Meneja
Biashara wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura)
amekutwa amekufa hotelini katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi
baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitoka Dodoma ambako alihojiwa
na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Meneja
huyo, Julius Gashaza, ambaye alikuwa na jukumu la kupanga bei za mafuta
za kila mwezi, alihudhuria kikao hicho mjini Dodoma kwa siku mbili;
Ijumaa na Jumamosi iliyopita kuhusu mambo mbalimbali, yakiwamo kiwango
cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na Ewura
kwenda kuhudumia umeme vijijini (Rea) na fedha za mfuko wa barabara.
Jeshi
la Polisi, Mkoa wa Temeke limethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa
meneja huyo alikutwa amejinyonga kwa kutumia tai kwenye hoteli ya Mwanga
Lodge iliyopo Yombo Vituka wilayani Temeke.
Nyumbani
kwa meneja huyo wa Ewura, kulikuwa na waombolezaji waliokuwa kwenye
vikundi na kikao cha maandalizi ya mazishi kilifanyika ndani ya nyumba
ya marehemu iliyopo Yombo Vituka na baadaye kuhamia nyumba ya jirani.
Kamati
ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew
Chenge, ilikutana na maofisa wa Ewura, akiwamo Gashaza na wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na kugundua kuwapo kwa tofauti katika takwimu za
kiwango cha mafuta kilichostahili kutozwa kodi.
Gashaza
alikwenda Dodoma kutoa ripoti ya Ewura kwenye kamati hiyo ya Bunge
akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo, takwimu za Ewura
ziliashiria kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi ya zile
zilizoelezwa na TRA, lakini Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe takwimu
za mamlaka ya mapato.
Habari
hizo, zinasema baada ya kurejea Dar es Salaam juzi majira ya saa tatu
usiku, Gashaza hakwenda nyumbani kwake na badala yake alikwenda kwenye
hoteli iliyo karibu na nyumbani ambako mkewe na ndugu yake mmoja
walimfuata na akawaeleza kuwa anahisi kutishiwa maisha yake.
Baadaye walifanya maombi maalumu kabla ya kuachana naye.
Inadaiwa
kuwa marehemu aliomba akalale hotelini kwa sababu hakuona kama ana
amani kulala nyumbani kwake na ilipofika asubuhi alikutwa ‘amejinyonga’
ndani ya chumba alicholala hotelini humo.
Nyumbani
kwa marehemu waombolezaji walikusanyika katika makundi, lakini baada ya
kukaa katika kikao cha familia walitoka na kauli moja kuwa hawatasema
chochote na kwamba jukumu hilo libaki mikononi kwa polisi.
Polisi wathibitisha
Kamanda
wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Seleiman Kova hakuwa tayari
kuzungumzia suala hilo akidai kuwa anayetakiwa kulizungumzia ni Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engbert Kiondo.
Alipotafutwa,
Kamanda Kiondo alisema kulingana na taarifa zilizopo Gashaza aliitwa
bungeni Mei 14 na akarejea Dar es Salaam Mei 17. Alisema aliporejea,
Gashaza aliaga nyumbani kwake kuwa hajisikii vizuri na kuelekea Hoteli
ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo ambako alichukua chumba Namba 113.
Kamanda
Kiondo alisema akiwa hotelini, Gashaza alimpigia simu rafiki yake mmoja
anayejulikana kwa moja la Silipwango akimweleza kuwa yupo hotelini hapo
kujipumzisha kwa sababu bungeni aliulizwa mambo ambayo hayakumpendeza
na kwamba alihitaji kupumzika.
Rafiki
huyo, kwa mujibu wa Kiondo, alimpigia simu mkewe anayeitwa Judith
akamweleza alivyoelezwa na mumewe na baadaye kwa pamoja wakamfuata
hotelini ambako baada ya kuzungumza nao kwa muda mfupi, aliwaomba
wamuache apumzike na ndipo walipoondoka.
Asubuhi,
Silipwango alipigiwa simu na mkewe kumueleza kuwa Gashaza hakurudi
nyumbani na akaamua kupitia kwenye hoteli waliyomuacha na alipofika
akakuta watu wamejaa. Alipouliza akaelezwa kuwa kuna mtu amejinyonga
chumbani.
Kamanda
Kiondo alisema Gashaza alijinyonga kwa kutumia tai aliyoifunga kwenye
bomba la maji ambalo pia lilikatika na hivyo kuukuta mwili wake ukiwa
sakafuni.
Kilichojiri kamati ya bajeti
“Kisheria
kodi ya mafuta ni Sh263 kwa lita inakwenda mfuko mkuu Hazina na Sh50
inakwenda kwa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), lakini takwimu za mafuta
yaliyouzwa inayostahili kutozwa kodi kati ya TRA na Ewura
zinatofautiana,” alisema mmoja wa wajumbe.
“Kwa
hiyo Kamati ya Bajeti iliwaita wote (Ewura na TRA) na kwa kweli wajumbe
wa kamati tulikuwa wakali sana, hatutaki mchezo tulitaka kujua nani
anasema ukweli,” alidokeza mjumbe huyo.
“Uko
ugomvi mkubwa tu kati ya TRA na Ewura kuhusu nani hasa mwenye takwimu
halisi,” alisema mjumbe huyo na kudokeza kuwa meneja huyo alisema kila
kitu kwa uwazi.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa baada ya vuta nikuvute ndani
ya kamati hiyo, iliamuliwa watendaji wa vyombo hivyo viwili wakafanye
ulinganisho na kupeleka jibu kwa kamati hiyo. Ewura waliwasilisha
takwimu zao Jumamosi.
“Tension
(mvutano) ni kubwa kwa sababu kuna watu wizarani hawazitaki takwimu za
Ewura na wanataka za TRA ambazo sisi kama wajumbe tunaziona hazina
uhalisia kunaweza kukawa na ufisadi,” alisisitiza mjumbe mwingine.
Chenge azungumza
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge alipoulizwa jana, alikiri
kufanyika kwa kikao kilichomuhusisha meneja huyo na kwamba taarifa
alizotoa zilionekana tofauti na zile za TRA.
“TRA
ni chombo cha Serikali na Ewura ni chombo cha Serikali, kwanini wawe na
takwimu zinazotofautiana? Hilo tu ndio tumewaagiza wakae pamoja
watuambie zipi ni takwimu halisi,” alisema Chenge.
Alipoelezwa
kuwa mmoja kati ya maofisa wa Ewura waliofika mbele ya kamati yake
amejinyonga, Chenge alionyesha kushtushwa na kuhoji kama taarifa hizo
zina ukweli.
“Una
uhakika kwamba amejinyonga? lini? Kama ni kweli basi ni jambo la
kusikitisha sana, lakini hiyo sasa ni kazi ya polisi. Mimi nisingependa
sana kuzungumza, tuwaachie wao wachunguze sababu za kifo chake,” alisema
Chenge.
Serikali
inaelezwa kuwa katika hali mbaya kifedha na kamati hiyo ya Bajeti
imekuwa ikifanya kila linalowezekana kuinusuru kwa kukutana karibu kila
siku na Hazina na wadau wengine wanaochangia fedha katika mfuko wake.
Kwa
bajeti ya mwaka 2013/2014 iliyopitishwa na Bunge, Serikali imejikuta
ikiwa na upungufu wa Sh1.8 trilioni hali ambayo kamati ya bajeti
inatafuta kila njia ikiwamo kushauri vyanzo vipya vya mapato ili
kunusuru bajeti ya mwaka huu wa 2014/2015.
Bajeti
ambazo zinaelezwa kuiumiza kichwa Serikali ni ya Maji, Miundombinu na
Nishati na Madini ambazo zinaelezwa kupata mgawo kidogo mwaka jana na
kuzifanya zishindwe kutekeleza miradi mbalimbali.
Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Godwin Samwel alisema alipata taarifa jana saa 3:00 asubuhi.
Alithibitisha kuwa marehemu alikuwa Dodoma kikazi kwenye vikao na kamati ya Bunge tangu Alhamisi iliyopita.
Baada
ya kumaliza kazi ndiyo ndiyo jana (juzi) alichelewa sana kurudi ndipo
alipoamua kujipumzisha kwenye nyumba ya wageni (iliyopo karibu na
nyumbani kwake) ambako alikutwa amefariki,” alisema Samwel.
Alisema marehemu alikuwa mwadilifu, mchapa kazi na asiye na tatizo lolote kazini na kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa.
Credit: Mwana
0 comments:
Post a Comment