Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba, jana liliridhia azimio la kuzifanyia marekebisho kanuni zake saba bila kuwapo kwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wamesusia Bunge hilo.
Marekebisho hayo ya kanuni yanaonekana
kuwa pigo kubwa kwa wajumbe hao wa Ukawa kwa vile sasa hawatapewa tena
fursa ya kufafanua maoni ya wachache badala yake watasoma tu.
Awali, Kanuni ya 33 ilikuwa ikitaka
mwenyekiti wa kamati kutumia muda wa dakika 60 kusoma taarifa yake
iliyokuwa ikijumuisha maoni ya wajumbe walio wengi na taarifa ya wale
walio wachache.
Lakini kanuni hiyo sasa imefanyiwa
marekebisho, ambapo mwenyekiti wa kamati atasoma tu taarifa ya walio
wengi na maoni ya walio wachache yatasomwa na mmoja wa wajumbe wa walio
wachache.
Kanuni hiyo ya 33(5) sasa itasomeka:
“Maoni ya wajumbe walio wachache yatasomwa na mmoja wa wajumbe ambao
hawakuunga mkono maoni ya wajumbe walio wengi kwa muda usiozidi dakika
30.”
Akiwasilisha maelezo ya Kamati ya Maadili
na Haki za Bunge, mjumbe wa kamati hiyo, Evod Mmanda, alisema kuwa
hakutakuwa na nafasi tena ya mjumbe kutoka kundi la wachache kutoa mambo
kichwani.
Mmanda aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, alisema maoni ya
wachache yaligeuzwa kuwa maoni ya kisiasa na kubeba hoja za kishabiki za
kisiasa. Alisema kuwa kutokana na marekebisho hayo, hakuna jambo
litakalokuwa halijajadiliwa kwenye kamati, ambalo litaruhusiwa kusomwa
na walio wachache ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.
Kanuni nyingine zilizorekebishwa ni
pamoja na ya 32, ambayo sasa inaruhusu mjumbe yeyote au kundi lolote la
wajumbe kupendekeza sura mpya kwenye Rasimu ya Katiba.
Rasimu iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ina Sura 17.
Kanuni nyingine zilizorekebishwa ni 35,
41, 60, 62 na 82 pamoja na sehemu inayohusu orodha ya yaliyomo katika
kanuni hizo za Bunge za mwaka 2014.
Akichangia hoja ya marekebisho hayo,
mjumbe wa Bunge hilo, Anjelina Samike alisema kwamba wajumbe kutoka
kundi la walio wachache walikuwa na maneno magumu na yasiyo na staha.
Kwa upande wake, Yusuph Singo alisema
nafasi waliyokuwa wakipewa walio wachache, hawakuitumia kutoa
ufafanuzi, badala yake waliitumia kujadili na kuibua mambo mapya.
Baada ya kupitishwa kwa marekebisho hayo, Sitta alisema kanuni hizo zitaanza kutumika mara moja.
Wajumbe wanaotokana na Ukawa walisusa
kuhudhuria vikao vya Bunge hilo wiki iliyopita kwa kile walichodai
kupinga ukiukwaji wa kanuni na matumzi ya lugha ya matusi, kejeli na
dhihaka.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment