banner

Thursday, May 29, 2014

Zitto Kabwe awajibu CHADEMA baada ya kumtuhumu kwa ufisadi

 
Hii  ni  kauli  fupi  ya  Zitto Kabwe  kujibu   tuhuma  za  kambi  ya  upinzani  zilizoelekezwa  kwake.....

"Nasikitika kwamba katika hali niliyonayo ya kumwuguza mama yangu naingizwa kwenye siasa za majitaka.

"Kampuni ya LekaDutigite inamilikiwa na wasanii. Gombe Advisors ni kampuni isiyofanya faida (Company limited by guarantee) na haina maslahi yeyote ya kibiashara.

"Wasanii wa Kigoma wamefanya kazi na TANAPA na NSSF, kazi ambazo zinajulikana na zipo. Leo mpigie simu mfanyakazi yeyote wa NSSF utasikia kazi ya wasanii hao.

"Kwa namna yeyote ile hii ni ishara ya kukosa ubinaadam maana waliyoyasema wanajua sina faida yeyote ya kifedha Leo wala kesho kwa LekaDutigite na Gombe Advisors.

"Kipindi ambacho mama yangu yupo mahututi, tena mjumbe wa kamati kuu ya chama chao, pole ninayopewa ndio hiyo. Hakuna namna ya kukosa ubinaadamu zaidi ya hivi.

"Hata hivyo, ni vema CAG afanye ukaguzi haraka sana na Mimi binafsi nitawajibika iwapo itaonekana kwa namna yeyote ile nina maslahi ya kifedha katika LekaDutigite na gombe advisors.."

HALIMA MDEE amlipua Waziri TIBAIJUKA bungeni

Adai anamiliki maelfu ya ardhi hapa nchini Wabunge wamshambulia, Makinda amuokoa, CCM waitisha kikao cha dharura kumnusuru
 
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amemlipua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kwamba anamiliki maelfu ya ekari za ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mdee ambaye ni Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alirusha kombora hilo jana bungeni wakati akisoma maoni ya kambi hiyo kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
 
Makombora hayo ya Mdee, yalimfanya Waziri Tibaijuka, kutumia muda mrefu zaidi kujibu mashambulizi badala ya hoja za wabunge wakati akihitimisha hoja yake.

Majibu hayo yalimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kila mara kumtaka Waziri Tibaijuka ajibu hoja za wabunge badala ya kujikita kumjibu Mdee, katika masuala yanayoonekana ni binafsi.

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA
 MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA
 
Waziri Tibaijuka, alisema kuwa Mdee amekuwa bingwa wa kuiba siri za serikali ikiwemo mwaka jana kuiba andiko la chuo kikuu na mwaka huu ameiba barua zake za siri alizomuandikia Waziri Mkuu.

Hoja za Mdee

Mdee, alisema Waziri Tibaijuka ana maslahi makubwa katika sekta ya ardhi ambapo anamiliki kiasi kikubwa cha ardhi maeneo ya Kigamboni na Kagera Wilaya ya Muleba ambako katika eneo la Kyamnyorwa ana hekta 800.
 
Kwa mujibu wa Mdee, mjini Bukoba, waziri huyo mwenye dhamana ya ardhi, anadaiwa kumiliki ekari 100 alizozipata kiujanja.
 
Alisema eneo hilo alilipata kwa kuwahamisha wamiliki halali kwa nafasi yake ya ukurugenzi wa UN-Habitat na baadaye ya uwaziri wa ardhi.
“Mheshimiwa Spika, linapokuja suala la migogoro ya ardhi, Waziri Tibaijuka anakosa “moral authority” katika kuutafutia ufumbuzi wa haki. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuliangalia upya suala lolote la ardhi ambalo waziri atajiingiza kwani nyuma ya sakata hilo kuna maslahi binafsi yake kama hili la Chasimba, na Kigamboni,” alisema Mdee.
Mbunge huyo alifichua siri nyingine ya umiliki wa ardhi ya waziri huyo katika eneo la Kigamboni ambako kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya na wa kisasa.
Alisema katika eneo hilo, Waziri Tibaijuka, kwenye ekari 50,934 zilizoongezwa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni, amejimegea maelfu ya ekari.
Alisema Waziri Tibaijuka aliongeza eneo la mradi kutoka hekta 6,494 zilizokuwepo awali hadi hekari 50,934.
“Hoja hapa ni je kati ya hekta zilizoongezwa 44,440, zinazomilikiwa binafsi na waziri ni ngapi? Hii haina siri, akikataa kusema wananchi wanaelewa ni ngapi, na hotuba ya mwaka kesho zitatajwa hapa bungeni,” alisema Mdee.
Alisema anaitaka serikali kuangalia upya mipango ambayo inatayarishwa na kusimamiwa na Waziri Tibaijuka na jinsi gani inatekelezwa kwa madai kuwa haaminiki tena.
Mdee alisema katika migogoro mingi ya ardhi, Waziri Tibaijuka amekuwa akitajwa kuhusika na katika mazingira hayo ni dhahiri kuna jambo limejificha, hivyo ni wakati mwafaka kuchukua hatua kabla ya majanga zaidi kutokea.

Mbunge huyo alimshambulia Tibaijuka, kwamba hawezi kusimamia wizara hiyo kwani hata kwenye nafasi aliyoachia Umoja wa Mataifa, aliondolewa kutokana na uwezo mdogo wa kufanya kazi.

Akizungumzia sarakasi za mradi wa Kigamboni, Mdee alisema mpango wa ujenzi wa mradi huo, umekuwa ukilalamikiwa sana na kutiliwa shaka na wananchi wa eneo hilo.

Mbunge huyo alisema mpango huo ambao unaelezwa kuwa wa serikali, sio sahihi kwani umevalishwa koti tu la serikali.
Kwa mujibu wa Mdee, ukweli huo unathibitika kutokana na mvutano uliopo kati ya wananchi wa Kigamboni wakiongozwa na mbunge, Dk. Faustine Ndungulile na Waziri Tibaijuka kuhusu kukiukwa kwa sheria ya mipango miji.
“Huu ni udhaifu mkubwa kwa upande wa utawala kwani ndio kinakuwa chanzo cha mgogoro usiokwisha na kusababisha hata kama kuna nia njema basi dhamira ovu inaanza kujitokeza wazi mbele ya uso wa jamii,” alisema.
Mbunge huyo alisema katika kikao cha bajeti mwaka jana, Bunge lilitoa mwongozo wa kumaliza mgogoro kwa kuitaka serikali kupitia kwa Waziri Tibaijuka, kukaa na mbunge na wananchi kumaliza mtafaruku huo, lakini hadi sasa kikao hicho hakijawahi kufanyika.
 
Kibaya zaidi Mdee alisema wizara imeandaa Master Plan bila kuwashirikisha wananchi kupata maoni yao kama sheria ya mipango miji inavyotaka.
“Mheshimiwa Spika, kambi rasmi inauliza je hayo maoni ya mwanzo yalikusanywa lini? Kama yalikusanywa mbona wananchi wanalalamika? Tunamtaka waziri atoe majibu ya kueleweka,” alisema Mdee.
Mbunge huyo ambaye jana alikuwa mwiba kwa Waziri Tibaijuka, alihoji kama kuna uhalali wa kuendelea na mpango huu kabambe pamoja na wakala wa kuendeleza mji wa Kigamboni.

Mgogoro wa ardhi Chasimba

Akizungumzia mgogoro wa Chasimba, Mdee alisema kwa muda mrefu wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiitwa wavamizi.
Lakini alisema ukweli unabaki kuwa kuna siri kubwa sana iliyojificha ya namna Kiwanda cha Wazo Hill kwa kutumia viongozi wa kijiji wa kipindi kuuza ardhi ya wananchi wakiwa ndani, kisha kubadilisha mipaka na hatimaye kiwanda hicho kupewa hati kinyemela.
Kwa mujibu Mdee, mahakama iliamua- wananchi wahame, lakini pia iliiagiza serikali kwamba wajibu wake katika mgogoro huu ni kuwapatia makazi mbadala.
Alisema amri hiyo ilishindwa kutekelezwa kwa madai ya ukosefu wa fedha na eneo la kuwahamishia.
“Mheshimiwa Spika. hatimaye ‘inasemekana’ wizara ilipata ‘eneo’ la ekari 1,000 ukilinganisha na ekari 630 za eneo la Chasimba, mchakato ulisababisha kuitisha kikao cha wananchi, waziri na timu yake na mthamini mkuu wa serikali na timu yake, walifikia muafaka wa wananchi kufanya tahmini na kulipa fidia wote waliotathminiwa ambao jumla yao ni 4096,” alisema.
Mdee alisema wananchi hao waliahidiwa kulipwa sh 15,000 kwa mita moja ya mraba, pamoja na viwanja mbadala.
“Mheshimiwa Spika, lakini katika kile kilichoonekana kuna harufu ya wizi na rushwa, katika kikao kilichofanyika baa kikiwahusisha Waziri Tibaijuka, Diwani wa Kata ya Bunju, Mwenyekiti wa Mtaa wa Basihaya, pamoja na inayoitwa ‘Kamati ya Wananchi’, wWaziri alisema wananchi hawatalipwa tena sh 15,000 kwa Square Metre, bali watapewa 5,000 ya kifuta jasho,” alisema.
Mbunge huyo wa CHADEMA, alisema kilichofanyika baadaye, waziri na timu yake walianza kutumia vitisho na kuwataka wananchi wafungue akaunti na kujaza fomu zisizo hata na muhuri wala nembo ya wizara, zikiwataka waandike namba zao za akaunti na kwamba wangekutana na pesa zao huko huko.
Na zaidi ya hiyo, wananchi hao waliambiwa asilimia 10 ya pesa watakayolipwa itakwenda kwenye Saccos, ambayo haijulikani ni ya nani, imeundwa lini na kwa madhumuni gani.
“Mheshimiwa Spika, mpaka sasa waziri akiulizwa tutajazaje fomu na kuandika akaunti ili tuingiziwe pesa ambazo hata hatujui ni kiasi gani, anajibu utakachokikuta hata kama ni 200 ndio halali yako,” alisema Mdee.

Dalili za wizi

Kwa mujibu wa nyaraka- ambazo kambi ya upinzani inazo, Mdee alisema kaya 4,096 zilizofanyiwa tathmini, kwa kiwango cha sh 15,000 kwa mita moja ya mraba, fedha iliyotakiwa kulipwa ni sh 47,368,357,520/-.
Alisema hiyo inathibitishwa kwa barua ya tarehe 8/11/2013, yenye kumbukumbu namba CBA 171/312/01 kutoka kwa Waziri Tibaijuka kwenda kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Alisema katika barua husika, pamoja na mambo mengine anampa taarifa waziri mkuu juu ya uhitaji wa sh 69,051,215,426 kama hitaji la fedha kwa zoezi zima la kulipa fidia kutwaa eneo la makazi mbadala, kulipanga eneo jipya kimipango miji, kupima viwanja na kuweka miundombinu ya msingi hususan barabara, maji, shule ya msingi, dispensari.
Mdee alisema kitendo kinachofanywa na waziri pamoja na uongozi wa Kiwanda cha saruji cha Wazo kumlazimisha Waziri Mkuu akubali deal hiyo ifanyike haraka, inatia shaka kwani huenda Waziri Tibaijuka atafaidika na mpango huo.
Mdee alisema kwa mujibu wa tathmini, kaya zilizofanyiwa tathmini, na kutakiwa kupewa viwanja mbadala ni 4,096, lakini wizara inataka kuvilipia viwanja 4,500 na vilivyosalia 404 vya ziada havijulikani ni mali ya nani.

Taasisi yenye mahusiano na Tibaijuka

Mdee, alizidi kumkaba koo Waziri Tibaijuka kwamba ana mahusiano na taasisi ya Tanzania Women Land Acces Trust- (TAWLAT) ambayo imo katika mchakato huu tata.
Alisema kuwa ushahidi unaonyesha kuwa waziri alikishauri kiwanda kuingia mkataba na taasisi hiyo ya TAWLAT kutoa elimu na kuendesha mazungumzo na viongozi na wananchi wa Chasimba juu ya mgogoro wao.
Kutokana na mazingira hayo, Mdee alisema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina shaka juu ya ushiriki wa shirika hilo katika mgogoro wa Chasimba pamoja na kazi nyingine za wizara.
Alisema kwenye mgogoro huo wa Chasimba, taasisi hiyo ililipwa sh milioni 300 na milioni nyingine 300 zilizotolewa na Halmashauri ya Kinondoni.
“Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya Waziri Tibaijuka, katika kazi hiyo taasisi hiyo ililipwa sh milioni 300 na katika mchanganuo niliouainisha hapo awali, wangelipwa sh milioni 500 kwa kazi hiyo. Nikiwa kama mbunge wa jimbo husika, nikuhakikishie kwamba hiyo taasisi haikufanya kazi yoyote,” alisema.
Mdee alisema kazi ya uthamini ilifanikiwa baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani na timu toka Wizara ya Ardhi kuja ofisini kwake kumuomba awasaidie kutuliza upepo kwani wananchi walikuwa wakiwarushia mawe.
“Mheshimiwa Spika, ilituchukua mikutano mikubwa si pungufu ya sita mimi nikiwa msemaji mkuu kuwaelimisha wananchi nia ya tathmini huku wakubwa hawa wakiwahahakikishia kwamba watalipwa 15,000 kwa square metre na kupewa maeneo mbadala. Hakukuwa na cha TAWLAT, wala Waziri Tibaijuka,” alisema.
Kutokana na sarakasi hizo, Mdee alisema kambi ya upinzani inaitaka Takukuru kufanya uchunguzi wa ushiriki wa TAWLAT kuhusu ushiriki wake wa shaka katika kazi kadhaa za Wizara ya Ardhi na wasipofanya hivyo, watawasilisha hoja binafsi- kuhusu sakata hili.

CCM wakutana ghafla

Katika hatua inayohusishwa na ugumu wa bajeti ya wizara hiyo, wabunge wa CCM walikutana ghafla ambapo pamoja na mambo mengine walijadili mwelekeo wa bajeti ya wizara hiyo.

Karibu wabunge wote waliochangia bila kujali itikadi, waliishambulia bajeti ya wizara hiyo na kutishia kuondoa shilingi.
Mbali ya wabunge wa CCM kutishia kuondoa shilingi, mawaziri wengi hawakuwemo wakati Waziri Tibaijuka anasoma bajeti yake na taarifa zinadai kuwa wamemsusia kwa vile amekuwa hashiriki kwenye bajeti za wizara nyingine kwa namna yoyote ile.

Mmoja wa wabunge wa CCM, aliliambia gazeti hili kuwa chama kimeweka msimamo wa kumnusuru Waziri Tibaijuka

SUGU amkaanga Zitto bungeni

Katika Hotuba yake ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya Wizara ya Habari,Utamaduni na Michezo aliyoiwasilisha Bungeni leo hii, Waziri Kivuli Joseph Osmundi Mbilinyi  maarufu  kwa  jina la  Sugu amemtaja Zitto Z. Kabwe kama Mmiliki wa Kampuni ya Leka Dutigite aliyofanya biashara isiyo halali na Mashirika ya Umma ya NSSF na TANAPA.

Sehemu husika ya Hotuba hiyo ni hii:

Mheshimiwa Spika, Tarehe 13 Agosti, 2012, Msajili Msaidizi wa Makampuni katika Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni (BRELA) alitoa Hati ya Usajili (Certificate iof Incorporation) kwa kampuni inayoitwa Leka Dutigite Limited. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, Leka Dutigite Ltd. ina ofisi zake katika ghorofa ya kwanza ya jengo la City House lililoko katika Mtaa wa Mkwepu, Dar es SalaaM. Mheshimiwa Spika,
sugu
 
Katiba, yaani Memorandum and Articles of Association, ya kampuni ya Leka Dutigite Ltd. iliyosajiliwa BRELA tarehe 13 Agosti, 2012 inaonyesha kwamba mwenye hisa nyingi katika kampuni hiyo ni kampuni nyingine inayoitwa Gombe Advisors Ltd. ya Dar es Salaam.
 
Kwa mujibu wa taarifa za kibenki ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imezipata, mnamo tarehe 10 Desemba, 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani ilihamisha jumla ya shilingi 12,200,000 kwenda kwenye akaunti na. 0150357447800 iliyoko CRDB Bank tawi la Pugu Road, Dar es Salaam, inayomilikiwa na Leka Dutigite Ltd. Hifadhi ya Taifa ya Saadani inamilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambayo ni shirika la umma. Siku moja baadae, fedha hizo zilitolewa kwa pesa taslimu kutoka kwenye akaunti hiyo.
 
Baada ya hapo, kati ya tarehe 14 Januari na 7 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa jumla ya shilingi 28,600,000. Fedha hizi zote ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu aitwaye Mchange (shilingi 3,600,000 tarehe 14 Januari, 2013) na Leka Dutigite (shilingi 25,000,000 tarehe 23 Januari na 7 Februari, 2013). Kufikia tarehe 7 Februari, 2013, fedha hizo zote zilikwishatolewa benki.

Mheshimiwa Spika,
Tarehe 28 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa shilingi 32,367,000 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Kwa mujibu wa taarifa za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo. Siku nne baadae, yaani tarehe 4 Machi, 2013, NSSF ilifanya malipo mengine kwenye akaunti ya Leka Dutigite Ltd., kwa mikupuo miwili, ya jumla ya shilingi 46,663,000. Siku hiyo hiyo, fedha hizo nazo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo miwili. Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu katika ya tarehe 10 Desemba, 2012 na 4 Machi, 2013, Leka Dutigite Ltd. ililipwa shilingi 119,930,000 kwa utaratibu huo huo wa ingiza na toa fasta. Kati ya fedha hizo, shilingi 12,200,000 zililipwa na TANAPA na shilingi 79,027,000 zililipwa na NSSF.

Mheshimiwa Spika,
Katika mazingira ya kawaida, sio kitu cha ajabu kwa mashirika ya umma kama NSSF na TANAPA kufanya biashara na watu au taasisi mbali mbali kama makampuni binafsi. Ukweli ni kwamba, kwa upande wa malipo yaliyofanywa na TANAPA, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imeweza kupata nakala ya mkataba unaohusu Maandalizi ya Filamu (Documentary) kwa Ajili ya Kuhamasisha Shughuli za Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa Kutumia Wasanii Kutoka Kigoma. Mkataba huo umesainiwa tarehe 5 Desemba, 2012, kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Leka Dutigite Ltd. na una thamani ya shilingi 12,200,000, kiasi kile kile kilicholipwa na Hifadhi hiyo.
 
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mazingira ya malipo haya sio ya kawaida. Hii ni kwa sababu ya uwepo wa kampuni ya Gombe Advisors Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, kampuni hii ilisajiliwa tarehe 24 Novemba, 2011. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, ofisi za Gombe Advisors Ltd. ziko kwenye jengo la City House, Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko ofisi za Leka Dutigite Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, wakurugenzi wa Gombe Advisors Ltd. ni Zitto Zuberi Kabwe ambaye kazi yake inatajwa kuwa ‘mchumi’, na Raphael Ongangi ambaye anatajwa kuwa ‘mchambuzi wa fedha na vitega uchumi’ (Financial and Investment Analyst). Bwana Ongangi aliwahi kutajwa na gazeti la kila wiki la —– la tarehe 26 Desemba 2013 kuwa ni mmoja wa washauri wa Zitto Zuberi Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi wake.

Mheshimiwa Spika,
Zitto Zuberi Kabwe sio ‘mchumi’ anayetajwa katika nyaraka za BRELA zinazoihusu kampuni ya Gombe Advisors Ltd. pekee, bali pia ni Mbunge, tangu mwaka 2005, wa Bunge lako tukufu. Kama Mbunge, Mheshimiwa Zitto Kabwe ni ‘kiongozi wa umma’ kwa mujibu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 1995. Sheria hii inawalazimu viongozi wa umma, wanapokuwa madarakani, kuwa “waadilifu, wenye huruma, utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya maadili ili kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa Serikali.”
 
Aidha, viongozi wa umma “… watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi kwa umma na haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu.” Vile vile, kuhusiana na maslahi binafsi, Sheria hii inaelekeza kwamba “… viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya.”
 
Mwisho, kuhusiana na maslahi ya umma, viongozi wa umma wanatakiwa, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, kupanga masuala yao “kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma.” Kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, Mheshimiwa Zitto Kabwe hajawahi kutangaza maslahi aliyonayo kwenye mikataba ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd. na NSSF na TANAPA.

Mheshimiwa Spika,
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge anayebanwa na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, bali pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC). Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. NSSF na TANAPA ni baadhi tu ya Mashirika ya Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa PAC.
 
Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia makampuni yake ya Leka Dutigite Ltd. na Gombe Advisors Ltd., amefanya biashara na TANAPA, shirika la umma analolisimamia kama Mbunge na Mwenyekiti wa PAC. Mheshimiwa Zitto Kabwe na wanamuziki washirika wake, kwa kutumia makampuni ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd., wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF.
 
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya ukiukwaji wa Sheria uliofanywa na viongozi wa umma na mashirika ya umma katika kashfa hii. Pamoja na maelezo yatayotolewa , Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na TANAPA na NSSF; msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi ya fedha hizo kwa kuzingatia masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika usimamizi wa fedha za umma. Aidha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifanye uchunguzi juu ya malipo na matumizi husika kwa kurejea masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria nyingine zinazohusika. Kwa upande mwingine, kwa kuwa suala hili linahusu mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa fedha za umma, Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye uchunguzi wake juu ya madai ya masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya maadili ya kiongozi wa umma ikiwemo yahusuyo utangazaji wa maslahi.

Mheshimiwa Spika;
Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inatoa rai kwa wanamuziki na wasanii wengine wote nchini kuwa waangalifu na watu wanaotaka kutumia umaarufu wao kama wanamuziki na wasanii kwa lengo la kufanikisha dili za kifisadi. Bila kuchukua tahadhari ya kutosha, wasanii hao wanaweza kujikuta wakipoteza sifa na umaarufu wao ambao wameujenga kwa jitihada zao wenyewe.

Wednesday, May 28, 2014

Wizara ya Ardhi, nyumba na mkazi Yazua Gumzo Bungeni

 
 
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka serikali kusitisha zoezi la ugawaji wa ardhi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi mpaka pale itakapobainika ni kiasi gani cha ardhi kilichopo kwa wawekezaji,ili kuepusha migogoro ya ardhi nchini ambayo inaendelea kusababisha vifo vya watanzania wasio na hatia
 
Hatua hii inakuja huku waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Profesa Anna Tibaijuka akikanusha vikalia uwepo wa migogoro ya ardhi kwa kile anachokiita ukosefu wa tekinolojia. 
 
Ni katika Mkutano wa kumi na tano kikao cha ishirini Halima Mdee Msemaji kutoka Kambi Rasimi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni waziri kivuli wa Wizara ya Ardh Nyumba na Maendeleo ya makazi anasimama na kusema tathmiini hiyo ikifanyika kwa kiasi kikubwa itapunguza migogoro miongoni mwa wananchi na wawakezaji hasa wa kigeni
 
Esther Bulaya ni Mjumbe kutoka kamati yaBunge Maliasili na mazingira kwa niaba ya kamati hiyo anasistiza kufuata kwa sheria katika kutoa vibali vya ujenzi wa magorofa nchini.

Tarehe 27 mwezi huu waziri mwenye Dhamana ya  wizara ya Ardhi nyumba na maendeleo ya Makazi Prof Anna Kajumulo Tibaijuka aliwasilisha makadirio ya Mapato na matumizi kwa wizara yake na akaomba shilingi bilioni 11.5 kwa ajili ya mishahara, matumizi mengineyo  bilioni 42.

Tanzania yadai kuwa Waasi wa M23 walitoka Rwanda

Tanzania kwa mara ya Kwanza imesema inayo uhakika kuwa waasi wa M23 walioondolewa nchini Jamuhuri ya Kongo  ni raia Rwanda. Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe ameliambia Bunge la Tanzania kuwa anao uhakika kuwa waasi   wa  M23 walitokea nchini Rwanda.
 
Hii ni Mara kwanza kwa Tanzania kukiri hadharani kuwa inao uhakika kuwa waasi hao ni raia wa Rwanda.
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimepeleka majeshi Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo kwa kushirikiana na yale ya umoja wa Mataifa yaliwaondoa waasi hao DRC

Waasi wa M23
Waasi wa M23

Matamshi hayo ya Waziri huyo aliyatoa wakati alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara yake ambapo pia alikiri kuwa bado uhusiano wa Tanzania na Rwanda sio mzuri.Hata hivyo upande wa Upinzani ulishambulia Waziri Membe  ukidai kwamba Waziri huyo anachochea kuvurugika kwa uhusiano wa Watanzania na Rwanda kwa kuhisi kuwa M23 ni Wanyarwanda nahata kutaka achukuliwe adhabu kali.

Mbali na tuhuma hizo Waziri Membe alizidi kusisitiza kuwa waasi wa M23 ni raia wa Rwanda akisema hiyo ni ripoti ya Umoja wa Mataifa.

Mbali na waziri,  baadhi ya wabunge walimuunga mkono waziri Membe kuwa waasi wa M23 ni raia wa Rwanda.

Wanachama SIMBA SC. wafunga barabara Msimbazi wakishinikiza WAMBURA kurudishwa kwenye orodha ya Wagombea

1
 
Mamia ya wapenzi na washabiki wa klabu kongwe ya mpira wa miguu hapa nchini Simba leo mchana wamejikusanya kwa wingi katika makao makuu ya klabu yao hiyo,kupinga Michael Wambura kuondolewa kwenye orodha ya wagombea kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
 
Wanachama hao ambao walizunguka jengo hilo na kutaka wapewe sababu za msingi kwanini Wambura ameondolewa huku wakitaka kufanya vurugu lakini vyombo vya usalama waliwahi kufika eneo la tukio na kuweza kuwatuliza wanachama Hao.
 
2
 
 Polisi wakiwa wamefika eneo la klabu ya simba ili kuimarisha ulinzi na kuwataka wanachama wa simba kutulia ili wapate majibu kwa kamati ya uchaguzi.
 
3
 
Wanachama wa simba wakiwa wamelizunguka Jengo la klabu yao mchana huu kupinga kuondolewa kwa wambura kwenye uchaguzi wa klabu hiyo

Kampuni ya GOOGLE waja na Teknolojia mpya ya Magari yanayojiendesha yenyewe..Cheki hapa

Gari linalotembea bila kuwa na dereva kutoka kampuni ya Google.
Gari linalotembea bila kuwa na dereva kutoka kampuni ya Google.

Kampuni ya Teknologia ya Google imetengeneza magari yanayojiendesha yenyewe.

Kampuni hiyo ambayo imejijengea sifa kwa njia ya kipekee ya utendaji kazi wake katika sekta ya kiteknolojia imekuwa ikikarabati magari ya kawaida.


Lina uwezo wa kumpeleka abiria bila kuwa na dereva.
Lina uwezo wa kumpeleka abiria bila kuwa na dereva.

Gari hilo la kiteknolojia halitakuwa na usukani.

Google imesambaza picha ya gari hilo ambalo inasema ni la kutumiwa mijini na linapaswa kuwa chambo kwa wale ambao bado hawana imani na teknolojia hii ya hali ya juu.

Mwasisi wa kampuni hiyo, Sergey Brin alizindua gari hilo la kipekee katika mkutano na wanahabari huko California.
Brin alisema kuwa teknolojia hiyo ina uwezo mkubwa wa kuimarisha maisha ya watu.

Mfumo wa gari hilo.
Mfumo wa gari hilo.

Watafiti wa magari yanayojiendesha yenyewe bado wanajadili iwapo kuwepo kwa magari hayo mabarabarani yatakuwa na upungufu wowote ikiwemo dhana kuwa itachangia ongezeko la msongamano wa magari.

Aibu! Mume wa Mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili Nchini ambaka mara 3 shemeji yake wa miaka 17..!!

Mume wa mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili, (jina tunalihifadhi kwa sasa), anatuhumiwa kumbaka shemeji yake mdogo (17).

Taarifa za tukio hilo ziliripotiwa juzi saa 12 jioni katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule), zikimtuhumu mwanamume huyo kwamba alimbaka binti huyo mara tatu na kumsababishia maumivu makali.

Binti huyo alifika katika kituo hicho cha polisi akiwa na ndugu zake wawili ambao walilalamika kwamba kulikuwa na jitihada kubwa kutoka upande wa mtuhumiwa wa kuzima kesi hiyo.
Akizungumza na gazeti hili nje ya kituo hicho, binti huyo alisema shemejiye alimbaka mara ya kwanza, Ijumaa iliyopita na Jumapili alipombaka mara mbili ndani ya gari.

Alisema mara ya kwanza alikaa kimya baada ya mtuhumiwa kumtishia kwamba angemdhuru kama angetoa taarifa ya tukio hilo alilofanyiwa wakiwa sebuleni nyumbani kwako Tabata Kimanga, lakini aliamua kutoa taarifa kwa ndugu zake baada ya kubakwa mara ya pili.

kova

Polisi katika kituo hicho walithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo lakini walishindwa kwenda kumkamata mtuhumiwa kwa maelezo kwamba hawakuwa na askari wa kutosha na kuahidi kwamba angekamatwa jana. Hata hivyo, hadi jana mtuhumiwa huyo alikuwa hajakamatwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi kutwa nzima ya jana hakupatikana kuzungumzia tukio hilo na kila simu yake ilipopigwa (kati ya saa nane mchana na saa mbili usiku), ilipokewa na msaidizi wake akisema bosi wake ana kazi nyingine.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hakuwa amepokea taarifa yoyote ya aina hiyo.

Mwimbaji anena

Alipoulizwa jana, mwimbaji huyo alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia kwa undani tuhuma zinazomkabili mumewe na kwamba alikuwa anajisikia vibaya kutokana na tukio hilo kuhusisha watu wake wa karibu.

“Of course (bila shaka), hili sio tukio zuri. Kwa sasa sina uwezo wa kuzungumza kwa sababu hili suala lipo Polisi. I am confused (nimechanganyikiwa), ukizingatia kwamba linasemekana kutokea wakati sikuwepo nyumbani, naomba tuzungumze baada ya akili kutulia,” alisema.

Kadhalika, jana saa 6:20 mchana, gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mtuhumiwa ambaye baada ya kupewa maelezo kuhusu tuhuma zinazomkabili alisema: “Samahani sana ujue sikusikii kabisa,” kisha alikata simu.

Gazeti hili lilimpigia tena simu lakini ilikatwa na baada ya hapo kila alipopigiwa haikupokewa. Baadaye saa 6:35 mchana, mtu aliyejitambulisha kuwa ni mdogo wa mtuhumiwa alipiga simu chumba cha habari akitaka kuonana na mhariri wa gazeti hili, kwa maelezo kwamba alipewa namba husika na kaka yake.

“Samahani, mimi (anataja ina) niko hapa nje Ofisi za Mwananchi, nilifika hapa kutaka kuonana na mhariri maana nasikia mwandishi wenu alikuwepo polisi tangu jana kwenye tatizo lililompata kaka yangu, sasa wakati nasubiri kuonana na mhariri kaka amenipigia simu akisema namba hii imempigia, kwa hiyo naomba tuonane ili tuzungumze tuone jinsi ya kumsaidia,” alisema.

Baada ya kuonana na mwandishi wa habari wa gazeti hili, alisema suala hilo lilikuwa likijadiliwa katika ngazi ya familia, hivyo wasingependa liandikwe kwenye vyombo vya habari.

Vipimo vya hospitali

Juzi, baada ya tukio hilo kuripotiwa, mtoto huyo alipelekwa katika Hospitali ya Amana ambako alifunguliwa faili la matibabu na kupewa namba ya usajili 667. Aliingia chumba cha matibabu namba 21 kumuona daktari kwa ajili ya vipimo zaidi.
Matokeo ya vipimo yalionyesha kuwa binti huyo alikuwa amefanya ngono kwa nguvu. Katika fomu hiyo ya uchunguzi, daktari aliandika ‘High vagina swab’.

Baada ya vipimo, familia ilirudi katika Kituo cha Polisi kupeleka matokeo ya vipimo vya daktari, hivyo kufungua faili la kesi lililopewa namba RB TBT/RB/319/2014 na namba TBT/IR/1865/2014. Jana binti huyo alikwenda tena Amana ambako alifanyiwa vipimo vilivyobaki vya VVU na mimba. Vipimo vya awali vya VVU vilionyesha kuwa hakuwa ameathirika na hakupata ujauzito.

Mtoto alipo

Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana jioni, zilisema mtoto aliyebakwa alichukuliwa na familia ya Mchungaji Josephat Gwajima.

Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Mchungaji Gwajima bila mafanikio, lakini lilimpata mkewe, Grace ambaye hakuwa tayari kuthibitisha kuwapo au kutokuwapo kwa mtoto huyo nyumbani kwake.

“Naomba nisiwe msemaji katika jambo hilo, yupo msemaji mwenyewe ambaye naamini mnamfahamu naye ni Mchungaji Gwajima, kwa hiyo mtafuteni, yeye atasema kama mtoto yupo hapa au hayupo na kama yupo sababu zake ni zipi,” alisema Grace.

Alipoombwa atoe mawasiliano ya simu ya mchungaji huyo, Grace alisema: “Kwa kweli kama unaweza, kesho nenda pale Kanisani Kawe utapewa utaratibu wa kuonana naye.”

Mama Mjamzito Afariki Dunia Kwa Kunywa SUMU

MAMA mjamzito aliyekuwa na mimba ya miezi tisa, Anjela Domiano (42), mkazi wa Nanenane katika Manispaa ya Morogoro, amefariki baada ya kunywa sumu ya panya.


Tukio hilo lilitokea juzi, saa 2.30 asubuhi, katika eneo la Kichangani katika Manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema jana kuwa, marehemu
Angela alifia katika hospitali ya mkoa, ambako alipelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Alisema siku ya tukio, Angela alikutwa akiwa ameanguka huku akitapatapa katika eneo la Kichangani.
 
Alisema polisi walipata taarifa na kufika katika eneo la tukio na kumchukua mama huyo na kumfikisha katika hospitali hiyo, ambapo alifariki wakati akipatiwa matibabu.
 
afande
 
“Wasamaria wema walipomwona mama huyo kaanguka chini, walitoa taarifa polisi na walipofika eneo la tukio, walimkuta akiwa anatapatapa na kuamua kumkimbiza hospitali ili kuokoa maisha yake,” alisema.
 
Alisema Angela alikutwa na sumu ya panya katika pochi yake na uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa, alifariki kutokana na kunywa sumu hiyo.
 
Kamanda huyo alisema hawakuweza kumhoji Anjela kutokana na hali yake kuwa mbaya na wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Mbunge wa NKASI anusurika kichapo bungeni baada ya kusema Zanzibar ni Mzigo

Kelele, kukunjana na kunyoosheana vidole jana mchana vilitawala nje ya ukumbi wa Bunge wakati wabunge wa CUF kutoka Zanzibar walipotaka ‘kumkanya’ Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.

Sakata hilo la aina yake lililodumu kwa takriban dakika 15 lilitokea saa 7:05 mchana baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha kikao cha Bunge.

Wabunge hao Mussa Haji Kombo (Chakechake), Kombo Khamis Kombo (Magogoni) na Muhammad Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe), walitaka ‘kumkanya’ Keissy kutokana na kile alichosema alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 2014/15 na kusema Zanzibar haichangii katika Muungano, hivyo haina haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili.

Kauli hiyo licha ya kulalamikiwa na wabunge wote wa CUF kutoka Zanzibar kiasi cha kufikia hatua ya kusimama na kuomba mwongozo wa Spika, Keissy alizidi kuwashambulia na kusema kuwa majimbo ya Zanzibar watu wake wanaweza kukusanywa sehemu moja kwa kupigiwa filimbi tu.

kessy

“Nyie Zanzibar idadi yenu ya watu ni asilimia 2.8 ya watu wote wa Tanzania. Sasa mnataka kupata kila kitu sawa ili iweje! Mnataka ajira asilimia 21 na Watanganyika wakafanye kazi wapi?” alisema Keissy.

Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho na wabunge kuanza kutoka nje, wabunge hao wa CUF walikwenda kumsubiri Keissy karibu na jengo la kantini.

Mbunge wa kwanza kumvaa Keissy alikuwa Khamis Kombo ambaye kabla ya kumfikia alizuiwa na Mbunge wa Mpanda Kaskazini (CCM), Moshi Selemani Kakoso.
Wakati Keissy akishangaa alitokea Haji Kombo ambaye naye alizuiwa na Mbunge wa Mikumi (CCM), Abdulsalaam Selemani Amer.

“Mimi sitaki kupigana bwana ninachokijua ni kwamba nilikuwa nikichangia mjadala wa bajeti na nilichokisema ni ukweli mtupu,” alisema Keissy huku akiwa amenyanyua mikono yake juu na kuondoka eneo hilo.

“Wewe (Keissy) sijui una nini wewe. Unapenda kutufuata fuata sana watu wa Zanzibar. Hivi una nini wewe? Hivi hujui kuwa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar?” alisikika akisema Khamis Kombo.
Kwa upande wake, Sanya hata baada ya wenzake kutawanyika eneo hilo, aliendelea kumlaumu Keissy na kuwataka wabunge wa CCM kumuonya.

“Anapenda sana kutoa kauli mbaya dhidi ya Zanzibar. Jamani mkanyeni mwenzenu haiwezekani kila siku awe yeye tu anayetukashifu bungeni,” alisema Sanya huku akitulizwa na mbunge wa Kibiti (CCM), Abdul Jabiri Marombwa.

Tuesday, May 27, 2014

Maji ya kuponya magonjwa yawa GUMZO…wenye Virusi vya vya Ukimwi wachekelea..!!

WANADAMU wanazidi kuegemea kwenye imani utata! Hivi karibuni, watu mbalimbali wenye magonjwa wamekuwa wakimiminika nchini Nigeria na kuoga maji ya bwawa yanayodaiwa yanaponya magonjwa papo hapo.

Watu hao wakiwemo wazee, vijana waume kwa wake na wenye magonjwa mbalimbali wamekuwa wakizama kwenye maji hayo kwa urefu wa futi tatu hadi nne, wengi wakiwa uchi au nguo za ndani tu.

Wengine huchota maji hayo na kuosha sehemu yenye tatizo hasa wale wenye kushindwa kuona au wenye vidonda sugu kama vile kansa, Ukimwi nakadhalika.

 
Watu mbalimbali wenye magonjwa  wakimiminika kwenye maji ya bwawa nchini Nigeria na kuoga  wakiwa na imani ya kuponywa magonjwa yao.
Watu mbalimbali wenye magonjwa wakimiminika kwenye maji ya bwawa nchini Nigeria na kuoga wakiwa na imani ya kuponywa magonjwa yao.

Bwawa hilo limepewa jina la Orimiri lipo umbali wa kilomita 3 kutoka mji wa Nachi, Enugu nchini humo na liligunduliwa na watu wa Kabila la Fulani.

Umati wa watu ukizidi kujitosa kwenye maji hayo huku wengi wao wakiwa utupu.
Umati wa watu ukizidi kujitosa kwenye maji hayo huku wengi wao wakiwa utupu.

Tangu kugunduliwa kwa bwawa hilo, zaidi ya watu 3000 wameshafika kuyaoga maji hayo kuanzia asubuhi hadi saa 12 jioni.
Hata hivyo, hakuna taarifa za moja kwa moja na uwazi kwamba watu wamepokea uponyaji.

Nigeria ni nchi yenye matukio mengi ya kiimani licha ya mambo ya kisiasa ambapo mpaka sasa wananchi wake wamekuwa wakikumbana nayo.


Wananchi wakiwa wamejaa bwawani kama kwa Babu wa Samunge.
Wananchi wakiwa wamejaa bwawani kama kwa Babu wa Samunge.

Baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakiwaambia waumini wao kuamini zaidi katika uponyaji wa Mungu.
Nchini Tanzania, miaka ya karibuni aliibuka Mchungaji Ambilikile Masapile ‘Babu wa Samunge’ akidai ana maji ambayo mtu mgonjwa akinywa anapata uponyaji.

Watanzania wengi, wakiwemo viongozi wa serikali walimiminika kwenye Kijiji cha Samunge, Loliondo kunywa kikombe chenye maji hayo lakini baadaye ilikuja kubainika kwamba, hakukuwa na uponyaji wowote zaidi ya kumwachia babu huyo utajiri.

Monday, May 26, 2014

Mkurugenzi wa zamani wa TANESCO afikishwa mahakamani kwa kosa la kuhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya milioni 884

 
                 Mhando (kushoto) na wenzake wakitoka mahakamani.

MKURUGENZI  wa zamani wa Shirika la Umeme nchini, (Tanesco) William Geofrey Mhando na mke wake, Eva Stephem Mhando, na maofisa wengine watatu wa shirika hilo, France Lucas Mcharange, Sophia Athanas Misidai na Naftali Luhwano Kisinga,  leo wamepandishwa kizimbani Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam kwa kosa la kuhujumu uchumi na kuiingizia serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 884,550,000. 
 
Katika kesi hiyo iliyosomwa na Wakili wa Serikali, Leonard Swai, mbele ya Hakimu Frank Mushi, wakili huyo alisema Mhando akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco anatuhumiwa  kumpa tenda mke wake ya kusambaza vifaa vya stationery vyenye thamani ya shilingi milioni 884,550,000/ kwa shirika hilo kinyume na taratibu.
 Waliounganishwa kwenye kesi hiyo nao wakishuka kizimbani chini ya ulinzi mkali.
 Mke wa Mhando (kushoto) na mwenzake wakirudishwa mahabusu.
 Askari kanzu akitanua njia wakati Mhando (mwenye shati jeupe) akipelekwa kizimbani.

Magazeti ya leo Jumatatu ya tarehe 26 May 2014


Majambazi waua Askari Polisi Temeke

Tahadhari: Picha zinatisha

Askari polisi mmoja wa kituo cha polisi Chang’ombe, Mkoa wa kipolisi wa Temeke, ameuawa kikatili siku ya Ijumaa mchana baada ya kupigwa risasi ya kifua na majambazi waliokuwa wanajaribu kutoroka baada ya kufanya tukio la kihalifu. 

Askari hao waliokuwa doria katika eneo la Wailes walijikuta wakishambuliwa kwa risasi na majambazi hao mara baada ya majambazi hao kujaribu kukimbia katika eneo la tukio kwa kutumia usafiri wa pikipiki kipindi ambapo askari polisi walikuwa karibu na eneo la tukio. 

Hata hivyo wakati askari hao wakijaribu kuwafukuza majambazi hao wawili kwa lengo la kuwakamata ndipo jambazi mmoja alitoa bastola na kumpiga risasi ya kifua askari huyo na kufariki pale pale.


Mwili wa askari huyo ukiwa umehifadhiwa.
Mwili wa askari huyo ukiwa umehifadhiwa.

Hata hivyo katika harakati za kujaribu kukimbia majambazi hao walianguka na pikipiki waliyokuwa wakitumia ndipo wakaamua kutimua mbio mitaani na kuingia katika nyumba moja ambapo walijificha na kujifanya kama ni wakazi wa eneo hilo, baada ya wnanchi na polisi kufika katika nyumba hiyo, baadhi ya majirani waliwaambia polisi kwamba wameona watu hao wameingia katika nyumba hiyo. 
 
Baada ya polisi kuingia waliwakuta watu hao wakiwa wametulia kama kwamba wao ni wakaazi wa nyumba hiyo na wala hawajui lililotokea.
 
Mwili wa mmoja wa majambazi ukiwa chumba cha kuhifadhia maiti
Mwili wa mmoja wa majambazi ukiwa chumba cha kuhifadhia maiti

Baada ya kuwatambua watu hao, polisi waliwatia nguvuni huku wananchi wenye ghadhabu waking’ang’ania kuwa wanataka kuwaua sababu wameshaua askari mmoja. Baada ya vuta nikuvute kati ya wananchi na askari hao ambao walikuwa wachache, wananchi walifanikiwa kuwachukua majambazi hao kwa nguvu kutoka mikononi mwa polisi na kuanza kuwapiga kwa silaha mbalimbali za kienyeji yakiwemo mawe na marungu mpaka watuhumiwa hao wakapoteza maisha.
 
4
Mwili wa jambazi mwingine ukiwa umeharibika vibaya baada ya kipigo kikali kutoka kwa wananchi wenye hasira.
Mwili wa jambazi mwingine ukiwa umeharibika vibaya baada ya kipigo kikali kutoka kwa wananchi wenye hasira.

Mwili wa askari polisi ukiwa umepakiwa kwenye gari ya polisi tayari kupelekwa hospitali ya Temeke kuhifadhiwa.
Mwili wa askari polisi ukiwa umepakiwa kwenye gari ya polisi tayari kupelekwa hospitali ya Temeke kuhifadhiwa.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo waliiambia blogu hii kwamba majambazi hayo kabla ya kupambana na polisi walikuwa wamefanya uvamizi na kumuibia mwanamke mmoja mkazi wa eneo hilo. Hata hivyo mali au fedha iliyoibiwa haikuweza kujulikana mara moja.

Kinana ainanga Serikali ya CCM

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ameainisha upungufu katika utendaji wa serikali na kueleza kuwa umesababisha wananchi kukilalamikia chama hicho mara kwa mara.

Kinana aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Peoples, ikiwa ni hitimisho la ziara yake mkoani Singida.

Alisema anatambua kuwa kuna upungufu na makosa ya kiutendaji kama kushamiri kwa rushwa na upendeleo serikalini jambo ambalo linasababisha wananchi kuilalamikia serikali na CCM.

“Watendaji serikalini wanatumia ufumbuzi wa muda wa kuzima moto, lazima tujenge utaratibu wa kumaliza matatizo ya wananchi kwa mipango ya muda mrefu,” alisema.

Aliongeza, “upungufu mwingine ni uwajibishaji wa watendaji wabovu, wakati anaharibu utawala bora haushiriki ila akishaharibu ndio utawala bora unaanza…”

kinana

“Inaundwa tume na uchunguzi kisa utawala bora, sipingi utawala bora bali napinga unaolalia upande mmoja… dhambi kabla haijatendaka hatua hazichukuliwi ila ukishakamilika ndiyo unachukuliwa,” alisema.

Alikosoa utaratibu wa kuwahamisha watendaji wanaotuhumiwa kwa utendaji mbovu na wizi, huku ikielezwa kwamba hakuna ushahidi wa kutia hatiani.

Kinana, alisema ni lazima nidhami iongezeke serikalini, uwajibishaji, kuchukua hatua mapema, na kwamba imekuwa kawaida kwa jambo dogo kuachwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na watu kwenye kituo kingine kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Wapo watendaji inawachukua muda mrefu kuchukua hatua,tutasimamia mapungufu ndani ya CCM na serikali yake,” alisema.

Aidha, aliwaahidi wananchi utumishi uliotukuka na siyo utumishi na kwamba kinachomshinda kushughulikia ni baadhi ya viongozi kupenda utukufu kwa kuitwa waheshimiwa bila utumishi uliotukuka.

Aidha, alisema alipokwenda kuna migogoro ya wakulima na wafugaji, wakulima na hifadhi, wakulima na misitu, wafugaji na hifadhi na wafugaji na misitu na kwamba Kamati Kuu, imeagiza kuchukuliwa hatua za kumaliza hatua zilizopo.
Alisema watendaji serikalini wanatumia ufumbuzi wa muda wa kuzima moto, lazima tujenge utaratibu wa kumaliza.

ATUMIA BAJAJI

Awali, Kinana, Naibu Katibu Mkuu wake, Mwigulu Nchemba na baadhi ya mawaziri, walitumia usafiri wa pikipiki na bajaji kuingia uwanjani hapo.

Mbali na mkutano huo, wananchi wakizunguzia ujio wa katibu huyo mkuu wa CCM katika mkoa wa Singida wanasema kuwa ni wazi kuwa uhai wa chama umerejea mahali pake kama ilivyo kuwa enzi za hayati Mwalimu Nyerere.

Magnalena Philemon mkazi wa Singida alisema CCM kilikuwa kimepoteza muelekeo lakini hadi sasa chama kimerudi mahali pake baada ya Kinana kuwepo madarakani.

Shabani Magita alisema CCM ni nzuri isipokuwa ‘imevamiwa’ na walafi na waroho wa madaraka waliokuwa wakitaka kukitumbukiza shimoni.

Mkuu wa mkoa huo, Dk. Perseko Kone, alisema wamepiga hatua kubwa ya kuondoka kwenye hali ya umasikini na balaa la njaa kupitia kilimo bora.

Alisema pamoja na juhudi za serikali, wamepiga hatua katika sekta ya elimu kwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi kwa asilimia 100.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Amosi Makala alisema serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha inaboresha na kukamilisha reli ya kati, ili usafirishaji mizigo na kukuza uchumi wa nchi.